LATEST POSTS

Wednesday, January 15, 2014

Nyalandu akejeli Bunge

Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amekejeli Bunge akidai taarifa kuhusu matatizo ya Operesheni Tokomeza Ujangili iliyotolea bungeni haikuwa na ukweli.
 
Kauli ya Nyalandu inaweza kuibua mvutano kati ya mihimili hiyo miwili ya Bunge na Serikali, na hivyo umma kuamini kwamba taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyochunguza suala hilo ilitoa ripoti ya uongo.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa James Lembeli, katika ripoti yake ilionyesha ushahidi wa vielelezo, zikiwemo picha za watu waliopigwa risasi na kuharibiwa sehemu za siri wakati wa kutekeleza operesheni hiyo ambayo imesitishwa kwa muda na serikali.

Kwa mujibu wa Nyalandu, kutokana na uongo uliopo kwenye taarifa hiyo, ndiyo maana Rais Kikwete amekubali kuunda tume ya kimahakama ambayo itawawajibisha wabunge na mawaziri waliosema uongo.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha mikoa ya Dodoma na Manyara juzi, Nyalandu alisema kutokana na kuenea kwa uongo wa taarifa hizo, kumekuwepo na hofu kwamba Tanzania huenda ikakosa fedha za Rais wa Marekani, Barack Obama.

Wakati Nyalandu akieleza suala hilo, waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia ndani, japo Tanzania Daima lilijipenyeza na kufanikiwa kupata kauli yake hiyo.

Naibu waziri huyo alifafanua kauli yake kwa wajumbe hao huku akitumia maneno aliyodai kuelezwa na mkewe kuhusu mjadala ambao uliibuka chuoni kwao ambapo wanafunzi wenzake walisema kuwa Bunge limesema uongo kwa Watanzania kuhusu kasoro ambazo zilijitokeza katika operesheni hiyo.

Alisema kuwa taarifa zilizotolewa juu ya operesheni hiyo hazikuwa na ukweli, na kwamba kutokana na hilo, taifa limeonekana kushuka kwa kasi katika masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kukithiri kwa vitendo vya rushwa.

Nyalandu aliongeza kuwa kwa sasa kuna mgogoro wa mipaka katika hifadhi ya taifa ya Tarangire, na kwamba amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na wabunge wa maeneo hayo pamoja na jamii yenye masilahi na maeneo hayo.

“Na nilikuwa najaribu kuzungumza na wenzangu ili tuangalie tufanye nini kwa sababu tumetoka katika Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo ilikuwa na kelele nyingi kwelikweli duniani, na sasa niliwaomba wenzetu wa Mkungunero ili kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro huo.

“Lengo ni kukaa kikao kama hiki kama mawaziri na watu wenye mamlaka na wahusika, ili tuweze kukaa pamoja kutatua migogoro,” alisema.

Nyalandu alitaka uamuzi wa kikao hicho ulenge kuwasaidia wananchi katika kutekeleza sheria za nchi.

“Lakini nataka kusema, jana nilikaa na mabalozi ambao wanawakilisha nchi zao hapa nchini, niliwaita ili niwape matokeo ya sensa ya mwaka 2007 hadi leo tumepoteza tembo kwa asilimia 66 na janga hili ni kubwa, unaweza kulitazama tu kiudhaifu, lakini imetokana na watu kuiona Tanzania kama shamba la bibi.

“Na nchi inapofikia mahali watu wakaanza kuwatukana viongozi, mtu anasimama anamtukana mkuu wa wilaya, akamtazama tu akamtukana mtu mwingine, akamtukana askari polisi…hii ni nchi pekee ambayo watu wanatukana viongozi na wanaachwa,” alisema.
Alisema kuwa aliwaeleza mabalozi hao kuwa Operesheni Tokomeza Ujangili namba mbili itarudi hivi karibuni baada ya kurekebisha kasoro.

“Sisi tulionewa kwa sababu ya maslahi, kwa sababu ya majukumu askari walifanya hivyo, jeshi lilifanya hivyo, wakuu wa mikoa walifanya hivyo.

“Aliniambia mtu mmoja kwa simu kutoka JST kuwa masuala ya rushwa Tanzania yamepanda juu mara moja baada ya Operesheni Tokomeza, kwamba ndipo wakakaa kikao na kusema hatuna hakika kama pesa za Obama zitatolewa, na mpaka sasa hazijatolewa,” alisema.

Lembeli amjibu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, amesema kuwa amesikitishwa na kauli ya Nyalandu.

Lembeli ambaye pia ni mbunge wa Kahama, alizungumza na gazeti hili jana kwa simu akisema amesikia kauli hiyo kwenye vyombo vya habari tu na kwamba kama ni ya kweli, basi Watanzania wana safari ndefu.

“Siamini kama matamshi haya kayatoa kweli kiongozi wa serikali ambaye bungeni siku hiyo alikuwepo na baada ya ripoti yetu sisi yeye anafanya utekelezaji wa ripoti yetu.

“Kawasimamisha kazi watendaji 22, hao wote ni kutokana na ripoti yetu, hadi kiongozi wa pori la akiba la Maswa yote hiyo ni kutokana na ripoti yetu, halafu leo aseme uongo, labda kama ana ajenda yake ya siri,” alisema.

Lembeli aliongeza kuwa kama Nyalandu atakuwa na hoja arudi bungeni na aseme kuwa ripoti hiyo ilikuwa feki ili kamati iweze kuudhihirishia umma ukweli uko wapi.

Aliongeza kuwa katika kamati hiyo hakuwa peke yake kwani walikuwemo hata wabunge wa upinzani pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga.

“Nasema hivi kama Nyalandu ana ajenda yake ya siri aseme na sio kubumba maneno tu kwani sisi tulienda kule ambako kunalalamikiwa na baadhi ya wabunge, kama kweli sisi tunasema uongo basi ukweli auseme yeye,” alisema.

Alisisitiza kuwa watu walifanyiwa vitendo vya kinyama na kumbukumbu za Bunge (hansard) zipo, kwa waliobakwa walikuwa wakijieleza na walikuwa wakirekodiwa, pia vielelezo vyote vipo na vinaonyesha.

 Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: