TAMAA
ya madaraka na fedha, vimetajwa kama sababu kubwa zilizowasambaratisha
wanasiasa wengi waliowahi kuvuma ndani ya vyama mbalimbali vya upinzani
nchini tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kisha
wakajisalimisha CCM.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa wakati Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kikitumia turufu hiyo kuwasambaratisha wanasiasa hao, wao
hujielekeza kufikiria zaidi vyeo na fedha.
Wako viongozi wengi waliowahi kuvuma ndani na nje ya nchi wakiwa
upinzani, lakini baada ya kurudi CCM, rekodi zao zimefifia kana kwamba
hawapo tena kwenye ulingo wa kisiasa.
Orodha hiyo ni ndefu, lakini kwa kutaja japo kwa uchache wako
wanasiasa kama Dk. Walid Aman Kabouru, Dk. Masumbuko Lamwai, Prince
Bagenda, Tambwe Hiza na Daniel Nzanzugwako.
Wapo pia Danny Makanga, Teddy Kaselabantu, Fatuma Maghimbi, Makongoro
Nyerere, Thomas Ngawaiya, Justin Sarakana, Frank Magoba na wengineo.
Hawa walipata kuwa viongozi ndani ya vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA,
CUF na TLP, lakini baada ya kusaliti upinzani na kurudi CCM walivuma
kwa muda mfupi kisha wakazimika kisiasa ikiwa ni pamoja na kushindwa
kura za maoni ndani ya chama.
Katika kuzungumzia anguko hilo, baadhi ya wanasiasa waliowahi kufanya
harakati za siasa na vigogo hao walitoa sababu kadhaa za kuporomoka kwa
wenzao.
Mabere Marando ni mwanasheria na Katibu Mkuu wa kwanza wa
NCCR-Mageuzi ambaye amefanya kazi za siasa na takribani wanasiasa wengi
waliotajwa hapo juu.
Katika mahojiano na gazeti hili, alitaja sababu tatu. Kwanza alisema
wakati wapinzani wanasaka vyeo na fedha CCM, malengo ya chama hicho
tawala ni kuwaangamiza kisiasa.
Marando ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, alisema
kuwa sababu ya pili ni kwamba umaarufu wa mpinzani hutokana na chama
pamoja na ukosoaji wa kutetea wananchi.
“Ukiwa CCM unatetea serikali si wananchi, ndiyo maana watu hawa wakienda huko wanapotea kabisa kisiasa,” alisema.
Katika sababu ya tatu, Marando alisema mpinzani akirudi CCM anakuwa
mgeni, kwamba wapo baadhi ya wanachama wasiopenda wanasiasa wanaorudi
huko wapewe vyeo, hivyo inakuwa vigumu kushirikiana nao.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare,
alisema kuwa siasa ni sawa na mchezo wa mpira wa miguu, ambapo CCM
hulazimika kuwachukua wanasiasa wenye nguvu na kushindwa kuwapa nafasi
katika chama hicho.
Lwakatare ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa upinzani bungeni
1995/2000, alisema kuwa hatua hiyo inasababisha wanasiasa waliohamia
chama hicho kupotea katika medali ya siasa kutokana na kukaa benchi.
Alisema kuwa umaskini umekuwa tatizo kubwa linaloathiri wanasiasa hao
kwa kuwa wanashindwa kuelewa suala wanalopigania kutokana na
kutanguliza maslahi binafsi.
“Hata hivyo, wanasiasa hao wanapotea kutokana na kutofahamu nyumba aliyohamia, anashindwa kuifahamu sawa sawa,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro,
alisema kuwa kuhama vyama kuna matatizo yake ambapo kunasababisha baadhi
ya mashabiki wako kushindwa kukuamini.
Mtatiro alisema kuwa mara nyingi mwanasiasa anakuwa na nguvu kutokana
na itikadi yake kwa wakati ule, lakini anapoondoka ndani ya chama hicho
hujikuta akipoteza wafuasi wote.
Alisema kuwa hatua hiyo inaweza kuwagharimu wanasiasa na hata
kuchukua kipindi kirefu kuweza kurudi katika nafasi ya juu waliyokuwa
nayo.
Rekodi za walioanguka
Masumbuko Lamwai:
Huyu aliwahi kuwa mbunge wa Ubungo (NCCR-Mageuzi), mwanasheria wa
chama kisha akarudi CCM na aliteuliwa kuwa mbunge, lakini sasa amepotea
kisiasa.
Danny Makanga:
Alikuwa mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), akavurugana na mwenyekiti
wake John Cheyo, kisha akavuliwa uanachama na kuhamia CCM. Sasa ni Mkuu
wa Wilaya ila kisiasa havumi tena.
Hiza Tambwe:
Alikuwa NCCR-Mageuzi kisha akagombea ubunge Temeke kupitia CUF. Huyu
alivuma na kuwahi kuapa kwamba kurudi CCM ni sawa na kulala na mama yake
mzazi, lakini leo yuko huko.
Alianza kupewa kitengo cha propaganda, lakini baadaye akaondolewa na
leo ni mwanachama wa kawaida wa CCM asiyekuwa na umaarufu kama zamani.
Thomas Ngawaiya:
Alianzia NCCR-Mageuzi kisha akageuka na Augustine Mrema kwenda TLP,
akachaguliwa mbunge wa Moshi Vijijini 2000/2005 kisha akarejea CCM.
Huko alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa Kilimanjaro, lakini
sasa ametupwa nje na hata alishindwa kura za maoni za kugombea ubunge wa
Moshi Mjini.
Dk. Walid Aman Kabouru:
Huyu alikuwa Katibu Mkuu CHADEMA na mbunge wa Kigoma mjini, lakini
akarudi CCM na sasa ni mwenyekiti wa chama Mkoa wa Kigoma ingawa
amefifia kisiasa.
Daniel Nsanzugwako:
Alikuwa Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi, baadaye akarejea CCM na
kushinda ubunge Jimbo la Kasulu Vijijini, kisha akateuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wakati wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri alitupwa nje na mwaka 2010
akadondoshwa jimboni na Zeituni Buyogela wa NCCR-Mageuzi, sasa havumi
tena.
Makongoro Nyerere:
Huyu ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Alivuma sana mwaka
1995 aliposhinda ubunge wa Arusha mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi.
Baadaye ubunge wake ulitenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha
kisha akarejea CCM na kuteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa mbunge
halafu akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara.
Kwa sasa Makongoro amepoteza nafasi hiyo ingawa ni mbunge wa Bunge la
Afrika Mashariki kupitia CCM, lakini nyota ya kisiasa imefifia.
Fatuma Maghimbi:
Huyu ni mbunge wa kwanza mwanamke wa upinzani kuchaguliwa jimboni
huko Wawi visiwani Zanzibar 1995/2005 kwa tiketi ya CUF, lakini baadaye
alirejea CCM na sasa amefifia.
Teddy Kaselabantu:
Alianzia UDP akiwa Katibu Mkuu na mbunge wa viti maalumu 2000/2005,
kisha akahamia CCM na kushinda jimbo la Bukene mkoani Tabora 2005,
halafu akashindwa kura za maoni 2010 na hivyo ikawa safari yake ya
kupotea kisiasa.
Prince Bagenda:
Huyu alivuma ndani ya NCCR-Mageuzi. Mwaka 1995 aligombea ubunge
Muleba Kusini na kushindwa kwa mizengwe na Wilson Masilingi wa CCM.
Mwaka 1997 matokeo hayo yalitenguliwa baada ya Bagenda kushinda kesi.
Hata hivyo wakati wa uchaguzi mdogo chama chake kilikuwa na mgogoro na
hivyo akashindwa kukidhi kigezo. Kwa sasa yuko CCM na kisiasa hakumbukwi
tena.
Frank Magoba:
Alipata kuwa mbunge wa Kigamboni kupitia CUF 2000/2005 kisha
akatimkia CCM na kugombea ubunge Mbeya vijijini ambako alikosa na sasa
kisiasa hajulikani tena.
Stephen Wassira:
Huyu pekee ndiye ameweza kuendelea kuvuma hata baada ya kutoka upinzani na kurudi CCM.
Alivuma akiwa NCCR-Mageuzi ambapo alishinda ubunge wa Bunda mwaka
1995, lakini baadaye akaenguliwa na Mahakama Kuu kufuatia kesi
iliyofunguliwa na mshindani wake Jaji Joseph Warioba.
Baadaye alihamia CCM ambako hadi sasa amekalia jimbo hilo vipindi
viwili huku akishika wadhifa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano
na Uratibu).
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment