MKOA wa Tabora umepiga marufuku viongozi wa kisiasa kuongoza vyama
vya ushirika vya wakulima kwa madai ya kutanguliza maslahi yao badala
ya kuwatetea wakulima.
Hayo yalibainishwa na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)
katika kikao kilichofanyika mjini hapa juzi, ambapo wajumbe hao
walisema wanasiasa wengi hawatetei maslahi ya wakulima ndiyo maana
matatizo yanayowakabili wakulima hayaishi.
Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba
(CCM), alisema baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaingiza siasa katika
masuala yanayogusa maslahi ya wakulima jambo linaloathiri maendeleo ya
vyama hivyo.
Alisema umaskini wa wakulima wa tumbaku hasa mkoani Tabora kwa kiasi
kikubwa umechangiwa na kuingiza siasa katika masuala ya kilimo, huku
akitolea mfano wa mauzo kufanywa kwa dola ya Marekani, mikataba ya
ujanja ujanja ya mikopo iliyojaa ulaghai.
“Naomba viongozi wote wa kisiasa ambao wapo kwenye uongozi wa vyama
vya wakulima ambao ni wenyeviti na watendaji wa vijiji au kata,
madiwani, wabunge na wengineo waachie ngazi,” alisema na kuongeza
kwamba Bunge limepitisha sheria mpya ya ushirika itakayoongoza masuala
yote ya vyama hivyo.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma
Mwassa, aliutaka uongozi wa vyama vya ushirika kuboresha mfumo wa
usambazaji pembejeo ili kumrahisishia mkulima upatikanaji wake.
0 comments:
Post a Comment