Mwenyekiti wa chama cha CUF , Profesa Ibrahim Lipumba.
Sintofahamu imeendelea kukigubika Chama cha Wananchi (CUF),
baada ya kauli ya mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba
kuwaacha wafuasi wa chama hicho katika giza nene juu ya hatima yake
kisiasa.
Hali hiyo ilitokea jana baada ya mkutano wa
Profesa Lipumba aliouitisha na wanahabari kuahirishwa bila kuelezwa
utafanyika lini badala yake akawaambia wafuasi wa chama hicho
waliokusanyika makao makuu wa chama hicho, Buguruni kuwa “kila
mwanachama ana wajibu wa kujenga chama bila kujali wadhifa wake.”
Makumi
ya wafuasi hao walitaka kusikia Profesa Lipumba akieleza mustakabali
wake baada ya kuripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa
amejiuzulu.
Hata hivyo, wazee wa CUF waliwahi kufika
katika ofisi ya mwenyekiti huyo na kumtaka awaeleze alichotaka
kuzungumza na wanahabari kwanza, kitendo kilichosababisha kuchelewa kwa
mkutano huo na kuvutia idadi kubwa ya wafuasi waliokuwa wakiimba...
“Kimyakimya, nguvu ya Lipumba mnaijua.” Wimbo mwingine ulikuwa... “Si si
si mnaona!! Nguvu ya Lipumba kuituliza hamuwezi.”
Baada
ya kuahirishwa kwa mkutano huo na wafuasi kuendelea kuimba, Profesa
Lipumba alitoka ofisini kwake saa 6.25 mchana na baada ya Msemaji wa
Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba kuwatuliza
wafuasi hao, Profesa Lipumba alizungumza nao akiwataka waisome na
kuielewa katiba ya CUF ambayo imewapa wajibu wa kukijenga chama chao.
Alisema mchakato wa kukijenga chama hautegemei wadhifa alionao kada husika, bali uanachama wake pekee unatosha kuleta maendeleo.
“Mwaka
1995 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipogombea urais kwa tiketi ya
CUF na mwaka 1999 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipoongoza kampeni za
Jimbo la Temeke na Ubungo ambapo tulishinda lakini wakatuibia kura,”
alisema.
Huku akionekana mtulivu tofauti na nyakati
nyingine anapozungumza na wafuasi wake, Profesa Lipumba alisema: “Chama
ni taasisi na tukijenge kama taasisi, ni wajibu wa kila mwanachama bila
kujali nafasi aliyonayo kukijenga,” alisema na kuhitimisha kwa salamu
ya; “hakiii” na kujibiwa “kwa wote,” bila kuimalizia.
Baadhi
ya wafuasi walionekana kutoridhishwa na kauli yake na kwamba ametumia
mafumbo wakati walitaka kusikia habari ya kujiuzulu kwake... “Kiu yangu
ilikuwa kumsikiliza baada ya kusikia fununu zilizoandikwa na gazeti jana
(juzi) badala yake katuambia tujitahidi kuendeleza chama,” alisema Said
Suleiman (58).
Hali ilivyokuwa
Mapema
saa nne asubuhi, wafuasi hao walianza kuingia taratibu katika eneo la
ofisi hizo na kujaa huku baadhi ya wazee wakiwa wameshaingia ofisini kwa
Profesa Lipumba.
Saa 6.05 mchana, Naibu Katibu Mkuu,
Magdalena Sakaya akiongozana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi,
Abdul Kambaya waliingia ndani ya chumba cha mkutano huku wafuasi wakiwa
wamejipanga mstari wakiimba nyimbo za kumsifu Profesa Lipumba na kusema
mkutano umeahirishwa hadi utakapotangazwa tena baada ya wazee, wanachama
na viongozi mbalimbali kuingia ofisini wakitaka kuelezwa fununu za
kujiuzulu.
Kuhusu taarifa za Profesa Lipumba kujiuzulu,
Kambaya alidai kwamba wanaosema hivyo wanapiga ramli na kwamba
yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni uzushi na hakuna matatizo
yoyote baina ya CUF na Ukawa na kama yangekuwapo, juzi Katibu Mkuu wake
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad asingehudhuria Mkutano Mkuu wa Chadema.
Katika
mkutano huo, Maalim Seif alisema hakukuwa na ukweli wowote juu ya
kujiuzulu kwa Profesa Lipumba na wanaosema habari hizo wanataka
kuwachafua na kuwavuruga Ukawa.
“Kiongozi yeyote
anayetaka kujiuzulu lazima barua yake atume kwa katibu mkuu wa chama.
Mimi sijapata barua yake na hadi jana saa nne usiku nilikuwa naye wala
hakuonyesha dalili za kujiuzulu,” alisema.
Lakini wafuasi waliokuwa wamepiga kambi CUF jana waligawanyika kimawazo juu ya ukweli wa taarifa hizo.
“Hofu
ya Profesa Lipumba kujiuzulu ipo, tena kubwa tu ndiyo maana tumekuja
kusikiliza lakini kwa sababu amekaa na wazee hakuna kitakachoharibika.
Ninaridhika CUF kuendelea kuwa ndani ya Ukawa ili upinzani tushike
dola,” alisema Mohamed Njuma kutoka Vingunguti.
Ismail Hamis alisema inaonekana kuna mgogoro hivyo wanataka kujua kilichomkumba kiongozi wao.
0 comments:
Post a Comment