LATEST POSTS

Thursday, August 6, 2015

Tuwakatae wanasiasa wenye roho ‘mtakavitu’

TANZANIA inaelekea pabaya na huenda ikawa mfano mbaya usiostahili kuigwa popote duniani katika suala la ushindani wa kisiasa. Maana halisi ya siasa imekosa utambuzi na badala yake imegeuzwa kuwa nyenzo ya chuki, fitina, uadui na kwa upande mwingine kitega uchumi (biashara) cha watu binafsi.
Maandalizi ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, yamedhihirisha wazi kuwa dhana ya demokrasia inaendelea kudhoofika badala ya kustawi katika vyama vya siasa nchini.
Wanasiasa waliojawa roho ‘mtakavitu’ wanapambana kwa ari ya kufa au kupona kupata uongozi ili kutumia nafasi hiyo kujineemesha na familia zao. Inashangaza kuona kuna wanasiasa nchini wanaoamini kimakosa kwamba bila kuwa rais, mbunge au diwani hakuna maisha tena Tanzania. Huo ni uroho wa madaraka.
Baadhi ya wanaowania uongozi wa kisiasa wamefikia hatua ya kushambuliana kwa matusi, ngumi na bakora hadharani wakati wa kujinadi kwa wapiga kura ndani ya vyama vya siasa. Wamesahau kwamba, siasa ni mchezo wa kushindana kwa sera na nguvu ya hoja.
Vitimbi vya kila aina vimeshika hatamu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao tofauti na uliopita. Unafiki, chuki, fitina, rushwa, kashfa, kuchafuana na kudhalilishana vimetawala kampeni za uchaguzi ndani ya vyama.
Cha kushangaza ni kwamba, baadhi ya wanasiasa wameonyesha unafiki mkubwa kiasi cha kuongopa mchana kweupe kwa lengo la kupata umaarufu na kuwadhoofisha kisiasa wapinzani wao mbele ya jamii. Ni katika kipindi hiki cha hekaheka za uchaguzi si jambo la ajabu kusikia mwanasiasa anajitoa fahamu na kuita rangi nyeusi kuwa ni nyeupe na nyeupe kuwa nyeusi.
Ukweli usiopingika ni kwamba, wanasiasa wanaocheza rafu hizi dhamira yao si ya kutafuta uongozi wa kuwatumikia wananchi. Kinachowasukuma zaidi ni hisia za kupata uongozi kwa ajili ya kuutumia kwa maslahi yao binafsi na familia zao.
Ndiyo maana kwa mfano, wanasiasa wengi katika mikoa ya pembezoni wanapochaguliwa kuwa wabunge huhama majimbo yao na kwenda kuishi pamoja na familia zao Dar es Salaam na Dodoma. Kwa mawazo yao potofu wanaamini hadhi ya mbunge haistahili kuishi jimboni na kujichanganya na wananchi wa kawaida, hususan wasiojiweza kiuchumi.
Lakini jambo la kujivunia ni kwamba Watanzania wa leo wamefikia hatua ya kutodanganyika tena. Ni watu wanaojitambua na wenye ufahamu mzuri juu ya kiongozi bora na bora kiongozi. Kwa hiyo, kipindi hiki hawako tayari kufanya kosa la kukubali kushawishiwa na chochote ili kuchagua kiongozi kinyume cha matakwa yao.
Yeyote anayeamini kimakosa kwamba ili achaguliwe kuwa rais, mbunge au diwani lazima apambane na wapinzani wake wa kisiasa kwa kuwajengea chuki, uadui, kuwatusi, kuwazushia kashfa na hata kupigana nao, atarajie suluba kali ya kisiasa kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Watanzania wanapenda kuona nchi inayosifika kwa tunu ya amani duniani inakuwa na wanasiasa wanaotambua kwamba, siasa ni ushindani wa sera na nguvu ya hoja. Pia wanataka kuongozwa na wanasiasa waadilifu, waaminifu, wenye hekima na uwezo wa kuongoza wasaidizi wao kutafuta ufumbuzi thabiti wa matatizo yanayowanyima maendeleo ya kweli kuanzia ngazi ya familia.
Umakini wa wananchi, hususan wapiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa kisiasa ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi katika taifa letu. Hata hivyo, hilo haliwezi kufikiwa ikiwa tutaendelea kuwakumbatia ‘wanasiasa maslahi’ wanaotafuta uongozi kwa kutumia mbinu haramu ili baadaye waugeuze kuwa kitega uchumi chao. Tuamke.

Chanzo: Raia Tanzania 

0 comments: