LATEST POSTS

Thursday, August 6, 2015

Dk. Slaa: Natishwa

 Slaa(2)

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, ambaye tayari amekwishakujivua uanachama wa chama hicho, amesema maisha yake binafsi pamoja na ya familia yake sasa yapo hatarini.
Hatua hiyo ya Dk. Slaa kufichua hatari hiyo inayomkabili dhidi ya maisha yake aliiweka bayana mwishoni mwa wiki katika mawasiliano yake na chumba cha habari cha Kampuni ya Raia Mwema Ltd, inayochapisha gazeti la kila wiki la Raia Mwema na gazeti hili la Raia Tanzania, linalochapishwa kila siku.
Slaa alilieleza Raia Tanzania kwamba kuna juhudi kubwa zinazofanywa na watu ambao hakuwa tayari kuwataja, akisema juhudi hizo zinalenga kutengeneza mizengwe ya kila aina na kisha kumdhuru, lakini hata hivyo, akisema haogopi chochote na kama ni “Mapenzi ya Mungu yatimizwe.”
“Ni dhahiri ninatengenezewa mizengwe ya kila aina. Inaonekana maisha yangu na ya familia yangu sasa yako hatarini. Nimekuambia (mwandishi wa gazeti hili) ili ikitokea chochote ujue siyo bahati mbaya. Sijawahi kuogopa na wala sitaogopa. Mtetezi wangu ni Mungu aliyehai na nina hakika atanilinda kama yanayopangwa siyo mapenzi yake. Kama ni mapenzi yake yatimie na isiwe kama ninavyotaka mimi,” alisema Dk. Slaa. 

Ilivyokuwa kujivua uanachama
Maisha ya Dk. Slaa yapo hatarini ikiwa ni takriban wiki moja tangu ajiuzulu wadhifa wake wa Katibu Mkuu Chadema na kisha kujivua uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Katika uamuzi wake wa kujiuzulu na kisha kujivua uanachama, Dk. Slaa pia aliweka bayana kwamba anastaafu shughuli za kisiasa, akifanya hivyo kutokana na uongozi wa juu wa Chadema kumkaribisha “kwa mizengwe” ndani ya chama hicho aliyekuwa kada wa CCM, Edward Lowassa, ambaye sasa ndiye mgombea wao pekee wa urais.
Dk. Slaa hakubaliani na namna Lowassa alivyokaribishwa Chadema bila kufuata utaratibu waliokubaliana ndani ya vikao vya chama hicho.
Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata wiki iliyopita zinasema, miongoni mwa mali za Chadema ambazo Dk. Slaa alizirejesha baada ya uamuzi wake wa kujiuzulu na kujivua uanachama, ni pamoja na gari alilokuwa akitumia kwa nafasi yake ya Katibu Mkuu. Mbali na gari hilo, alirejesha pia nyaraka nyingine za chama hicho.
Raia Tanzania lilipata taarifa za kurejeshwa kwa mali hizo za Chadema na kupiga kambi Ijumaa iliyopita, maeneo ya Ofisi za Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam hadi liliposhuhudia tukio hilo la kihistoria.
Majira ya saa 3.15 hivi, gari aina ya Noah lenye namba za usajili T 217 BUZ liliingia katika Ofisi za Chadema likiwa na watu wawili na gazeti hili liliwashuhudia wakiteremka na mkoba mwekundu na kisha kuingia ofisini.
Wakati huo nje ya ofisi, kulikuwapo pikipiki moja iliyokuwa ikizunguka Mtaa wa Ufipa kana kwamba inafanya doria.
Baada ya muda mfupi, saa 3:20 hivi, watu hao walitoka nje ya Ofisi ya Chadema wakiwa mikono mitupu, wakaingia kwenye gari lao na kuondoka eneo la Ufipa. Raia Tanzania lilishuhudia pikipiki hiyo iliyokuwa ikifanya doria ikiingizwa ofisini humo muda mfupi baadaye.
Kuhusu kurudisha kadi yake ya uanachama wa Chadema Ijumaa usiku, Dk. Slaa aliliambia Raia Tanzania akisema: “Sikuwahi kurudisha kadi ya CCM, kwa nini nirudishe kadi ya Chadema? Kadi ni mali yangu na hili nimekuwa nikilieleza mara kwa mara.”
Mbali na kauli hiyo ya Slaa, moja ya vyanzo vyetu vya habari kutoka Makao Makuu Chadema kilieleza; “Hilo sasa ni suala ambalo confirmed (ni rasmi). Dk. Slaa amejivua nafasi yake ya Ukatibu Mkuu na kujivua pia uanachama wa Chadema. Amekerwa na namna mambo yalivyofanyika hovyo, bila kujali misingi ya utawala na maadili katika chama.” 
Dk. Slaa aliacha uanachama wa CCM na kuingia Chadema mwaka 1995 baada ya kutoridhishwa na mchakato wa kusaka wabunge ndani ya chama hicho.
Mwaka huo 1995 alishinda ubunge kupitia Chadema na kudumu bungeni hadi mwaka 2010 alipogombea urais na kushika nafasi ya pili nyuma ya Rais Jakaya Kikwete, huku matokeo ya kura za urais yakigubikwa na tuhuma za uchakachuaji.
Tangu gazeti hili lilipoweka hadharani wiki iliyopita ukweli kwamba mwanasiasa huyo anayekubalika zaidi nchini ameacha nafasi ya Katibu Mkuu wa Chadema, kumekuwa na uzushi mwingi katika mitandao ya kijamii nchini.
Uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wake Chadema kwa kutoridhishwa na kupokewa kwa Lowassa kwenye chama hicho bila masharti, umefuatiwa na juhudi kubwa kutoka kwa watu mbalimbali kukanusha taarifa hizo kwa malengo ambayo hayajaeleweka wazi, lakini Ijumaa Dk. Slaa aliliambia Raia Tanzania kwamba ameamua kukaa kimya na kutojibizana na watu hao, asije akawa kama wao.
“Nimezoea kusimamia maadili ninayoyaamini. Nimeheshimu na kutii dhamira yangu daima kwa kuwa naamini Mungu huzungumza nasi kupitia dhamira zetu ndiyo maana binadamu tuko tofauti na viumbe wengine. Watasema mengi, propaganda daima hazijengi,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Wanaotumia propaganda kuhalalisha uamuzi mbovu, hawajui madhara wanayoyasababisha.
“Nitakuwa sina tofauti na wao nikipoteza muda kujibu kila kinachoandikwa kwenye mitandao. Nakuhakikishia sitakwenda chama kingine, bali nimestaafu siasa ili nitumikie taifa langu kwa njia nyingine,” alimwambia mwandishi wetu.
Akizungumzia taarifa zilizozagaa kwamba angezungumza na waandishi wa habari, Dk. Slaa aliliambia Raia Tanzania kwa kifupi: “Sina mpango huo, sina papara, najua kuna mengi yatasemwa. Wakati ukifika nitayazungumzia.”
Kutokana na uamuzi huo wa Dk. Slaa ni dhahiri sasa Chadema kinakabiliwa na wakati mgumu wa kusaka mrithi wa Katibu Mkuu huyo wa zamani aliyekuwa amekifikisha chama hicho katika kilele cha siasa Tanzania, na tayari watu wa karibu na Lowassa wameanza kujipanga kwa ajili ya kuinasa nafasi hiyo ya Katibu Mkuu. 

Makongoro Nyerere ashangaa
Katika hatua nyingine, mmoja kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa akiwania kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Makongoro Nyerere, amesema Chadema kitapata wakati mgumu kumsafisha mgombea wao wa urais, Edward Lowassa.
Makongoro na Lowassa ni miongoni mwa makada 32 wa CCM waliokatwa majina yao na Kamati Kuu ya chama hicho mjini Dodoma mwezi uliopita.
Akizungumza na Raia Tanzania jana, Makongoro alisema uamuzi wa Lowassa kuhamia Chadema ni wa kidemokrasia na haki ya kila Mtanzania.
“Huo ni uamuzi binafsi, uheshimike. Lakini chama chake kipya kitapata wakati mgumu sana kumsafisha kutokana na tuhuma za ufisadi anazoandamwa nazo.
“Chadema walikubalika mioyoni mwa wananchi kutokana na hoja ya ufisadi dhidi ya Lowassa. Hiyo sabuni au brashi ya kumsafisha haipo hata Nakumatt,” alisema Makongoro, mmoja kati ya wanaCCM wachache waliokuwa wakimnyooshea kidole Lowassa wakati wa kusaka wadhamini ndani ya chama hicho.
Kuhusu uamuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa kuachana na siasa, Makongoro alisema hilo si jambo jema hata kidogo.
“Tuna muhitaji. Taifa linamuhitaji. Wanasiasa wa aina yake wanatakiwa kuendelea kutoa mchango kwa mustakabali mwema wa taifa letu. Ninamshauri asiache siasa, aje CCM tujenge taifa,” alisema. 

Chanzo: Raia Tanzania

0 comments: