Umoja usio rasmi wa vyama vinne vya
upinzani nchini Tanzania unajulikana kwa jina la Katiba ya Wananchi
(UKAWA), baada ya kusubiri kwa muda hatimaye umemtangaza Waziri Mkuu wa
zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Lowassa
anagombea kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku
vyama vingine vitatu vikimuunga mkono. Hii inatokana na sheria za
Tanzania ambayo haitambui umoja wa vyama.
Kabla ya kujiengua chama
Tawala chama cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa amekuwa mwanachama wa
CCM kwa muda wa miaka 38, ambapo alijiunga na chama hicho mara tu baada
ya kumaliza elimu yake ya chuo kikuu mwaka 1977.
Hatua ya
mwanasiasa huyo mashuhuri nchini Tanzania kuamua kujiunga na chama cha
upinzani Chadema, ikiwa imebaki miezi mitatu tu kuelekea uchaguzi mkuu,
kumebadilisha kabisa upepo wa kisiasa nchini Tanzania, na hasa uchaguzi
mkuu ujao.
Lowassa alikuwa Maziri Mkuu
kati ya mwaka 2005 na 2008 kabla ya kujiuzuLu wadhifa huo kufuatia
sakata la kashfa ya rushwa iliyohusisha kampuni ya kuzalisha umeme ya
ki-Marekani Richmond Development Company LLC ya Houston Texas.
Hata
hivyo wakati anatangaza kuhamia kwake Chadema, Lowassa alikanusha katu
katu kuhusika kwa namna yoyote na kashfa hiyo na kudai kuwa yeye
alifuata tu amri kutoka kwa ‘wakubwa’ walio juu yake.
“Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa
Kuhama kwake kunamfanya Lowassa
kuwa ndie kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kabisa wa CCM kukihama
chama hicho tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mnamo
mwaka 1992.
Mwanajeshi wa zamani na aliyewahi kupigana wa vita
kati ya Uganda na Tanzania mwaka 1978/79, Lowassa aliiambia hadhara
kwamba akiwa kama mtu mwenye uchungu na nchi yake isingekuwa rahisi
kubaki ndani ya CCM huku akiona chama hicho kimepoteza mwelekeo na sifa
ya kuongoza nchi.
Lowassa amekimbilia upinzani baada jina lake
kukatwa wakati alipoomba kuwa mgombea urais kupitia chama tawala CCM
katika uchaguzi mkuu ujao utakafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Wakati
mchakato wa CCM wa kumtafuta mgombea wao wa urais ulipoanza, Lowassa
ndiye aliyekuwa kinara wa wagombea wote 42. Kila kona aliyozunguka,
mikutano yake ya hadhara ilivutia maelfu ya watu waliomuunga mkono.
Wakati
chama cha CCM kilimtaka kila mgombea apate sahihi za wadhamini 450
lakini Lowassa alipata sahihi za wadhamini zaidi ya 700,000.
Hata hivyo mchujo wa chama
ulipofanyika jina lake lilikatwa mapema kabla hata ya kupelekwa kwenye
vikao vya vya juu vya chama hicho. Ambapo baadae Waziri wa Ujenzi John
Pombe Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea na kuwa mgombea kupitia chama
tawala CCM.
Lowassa ameushutumu mchakato CCM wa kutafuta mgombea
urais akiuita kuwa ulijaa chuki na mizengwe dhidi yake, hali ambayo
aliifananisha na ‘ubakaji wa demokrasia’
“Nitakuwa mnafki nikisema
bado nina imani na CCM. CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia”,
alisema, na kuongeza “kama Watanzania hawapati maendeleo kupitia CCM
basi wakayatafute nje ya CCM”
Wakati sakala la Richmond
lilipoibuka miaka michache tu iliyopita, Chadema ilimfanya limsakama
Lowassa kuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa nchini. Lakini wakati chama
hicho kinamkaribisha kuwa mwanachama wao, kiligeuka na kusema hakuna mtu
msafi nchini na kwamba hawawezi kuacha kumpokea mwanasiasa mwenye mtaji
mkubwa wa wafuasi kama Lowassa.
Wakati akiwa Waziri Mkuu, Lowassa
alisifika kama mchapakazi hodari na msimamiaji wa moja kwa moja wa
shughuli za serikali. Bado anaendelea kufahamika kwa jina la utani la
‘mzee wa maamuzi magumu’.
Moja ya mafanikio makubwa ya
uwaziri mkuu wake ni jitihada kubwa na mafanikio ya upatikanaji wa fedha
za kujenga chuo kikuu cha Dodoma. Chuo hiki kikuu cha umma kilichopo
katikati ya Tanzania kilianzishwa mwaka 2007.
Lowassa ni mashuhuri
pia kwa kusimamia mpango wa serikali uliofanikiwa wa ujenzi wa shule za
kata ambazo uliiletea Tanzania sifa kubwa kwa kutoa fursa ya watoto
wengi kupata nafasi shuleni.
Mtoto wa Mzee Ngoyai Lowassa, ambaye
aliwahi kuwa mtumishi wa serikali ya kikoloni, Lowassa ameanza harakati
zake za kuwania urais tangu mwaka 1995 lakini inaarifiwa kwamba rais wa
kwanza wa Tanzania Mwl Julius Nyerere alimkatalia kushika nafasi hiyo.
Wafuasi wa Lowassa wamekuwa wakiyatupilia mbali madai hayo
Ulipofika
uchaguzi wa mwaka 2005, Lowassa hakutaka kuwania urais, lakini badala
yake alimnadi rafiki yake wa siku nyingi Rais wa sasa Jakaya Kikwete
ambaye alipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 80.
SOURCE: BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment