Mti ambao gari liliugonga kwa juu kabla ya kupinduka.
Akizungumza na Uwazi
mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ofisi ndogo ya chama hicho nyumbani
kwa marehemu, Mikocheni B jijini Dar, Mluya alisema hata watu waongee
vipi, lakini uchunguzi wao umeonesha kwamba, kiongozi wao aliuawa
tofauti na eneo la ajali na mwili kwenda kutupwa pale.
ROHO YAKE ILIWINDWA KWA SIKU 40
Mluya alisema: “Ndugu mwandishi,
Mchungaji Mtikila kama kufa alikuwa afe muda mrefu sana pengine siku
arobaini zilizopita (mpaka siku ya kifo cha kweli), kwa sababu amewindwa
na watu ambao hatujajua lengo lao kubwa lilikuwa nini!
“Kila alikokwenda kwa shughuli za kichama kulikuwa na timu ya watu inayomfuatilia.”
...Baada ya Kupinduka
MARA YA KWANZA
“Tarehe siikumbuki, lakini ni Septemba
mwanzoni. Tulikuwa Bunda, Mara kwenye shughuli za chama, kuna watu ambao
walikuwa hawaeleweki walitufuata mpaka hotelini.
“Baada ya kubaini hilo, nilimuuliza mwenyekiti kuhusu ratiba aliyokuwa nayo ya kuzungumza kwenye runinga ya Staa TV.
“Alinipa ratiba. Baada ya kumaliza
kuzungumza, nilimwambia Bunda si mahali pa kulala hivyo nilimshauri
aondoke, aende Mwanza. Na nilimwambia dereva wake aondoke bila kuaga.”
WAKIWA NJIANI
“Lakini cha ajabu, wakiwa njiani
wakielekea Mwanza kuna gari liliwafuata kwa nyuma kwa mwendo ambao
waliutulia shaka. Dereva wa mwenyekiti alipokuwa akiongeza mwendo, naye
anaongeza, akipunguza naye anapunguza.
“Ilibidi dereva amwambie mwenyekiti naye akamtaka dereva aongeze kasi hadi Mwanza.”
“Katika ratiba yetu tulitaka kufanya
ziara za kichama kuanzia Oktoba 18, mwaka huu kwa kuanzia mkoa wa
Kigoma na kwingineko. Pamoja na kufuatiliwa kote kule mwenyekiti hakuwa
na roho ya uoga hata kidogo. Alimtanguliza sana Mungu.
“Kwa hiyo wasiwasi mkubwa wa kufuatiliwa na watu hao ulianza Mara na Mwanza kwa nyakati tofauti.
“Septemba 11, mwaka huu ndiyo tarehe
ambayo sasa nilianza kukariri matukio hayo hatua kwa hatua. Siku hiyo
tulikwenda kwenye Kijiji cha Usangu mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya
kampeni ya mgombea udiwani. Baada ya kumaliza tuliamua kurudi Dar lakini
njiani dereva akasema kuna watu hawajui wanakuja nyuma yetu.”
WAPOTEA NJIA KWA KUFUATILIWA
“Tulijikuta tukipotea njia na kutokea
mjini Kisarawe (Pwani). Pale tulifika kituo cha mafuta ambapo tulikuta
gari aina Toyota Land Cruiser VX limepaki kama vile ni watu pia walikuwa
wakitufuatilia.
“Lengo la kusimama pale lilikuwa kupata
chakula lakini hatukufanya hivyo kulingana na mazingira. Tukaanza safari
ya kurudi Dar. Tulipofika Pugu Sekondari, gari lile lilitupita kwa kasi
na kupotea.
“Tulipofika Tazara gari lile lilionekana
na wakati huo yalikuwa mawili. Kilichotushangaza ni upya wa magari
lakini eti namba zinaanzia na A. Mimi nilifikiria kwamba, pengine ni za
idara ya usalama wa taifa zilikuwa doria mbalimbali hasa kipindi
hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Ndugu mwandishi, mimi ninafanya kazi ya siasa, niko makini sana. Niliwaambia wenzangu kuwa tunafuatiliwa.
“Ndani ya gari sisi tulikuwa na viongozi
wa kuwapeleka Temeke. Lakini baada ya kufika huko lile VX tulikutana
nalo. Tulipomuacha yule tuliyempeleka kule, tukawa tunampeleka mchungaji
nyumbani kwake (Mikocheni) lakini bado lile gari lilikuwa
likitufuatilia.”
WAPIGA CHENGA
“Tulipofika maeneo ya Msasani kwa
Mwalimu (Julius Nyerere) dereva alikunja kona kuelekea kwa mchungaji na
lile gari likakunja kona na kurudi lilikotoka.”
SIKU NYINGINE
“Siku iliyofuata tulipanga mipango yote
ambapo sasa tulisema Oktoba 18, mwezi huu tuanze ziara ya mkoa wa
Kigoma na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.
“Mimi niliondoka kuelekea Shinyanga,
yeye (Mchungaji) aliandaa safari ya kwenda Njombe kwenye kampeni ya
mgombea Ubunge Jimbo la Njombe.”
OKTOBA 2, 3, 2015
“Mwenyekiti aliondoka Dar Oktoba 2,
kuelekea Njombe. Oktoba 3, alinipigia simu asubuhi na kunijulisha kuwa
jana yake walipata ajali maeneo ya Makambako wakati wanakwenda.
“Nilimuuliza alipata matibabu, akajibu kuna viongozi wa Njombe walifika na kumchukua hivyo yuko sawasawa.”
TAARIFA YA AJALI
“Siku hiyo hiyo walifanya kampeni na
jioni yake walianza safari ya kurejea Dar. Walipofika Mkoa wa Pwani, saa
kumi na moja alfajiri, Mchungaji Mgaya alinipigia simu na kuniambia
walikuwa njiani wanarudi Dar, wamepata ajali mbaya sana. Lakini
hakuniambia kama mchungaji amefariki dunia.
“Nilianza kufuatilia tukio hilo na
kuuliza kama kuna msaada wowote wameupata, akasema mpaka muda huo polisi
walikuwa hawajafika. Mimi napenda sana kufungua mitandao ya kijamii,
nilipofungua nikakuta picha zilishasambaa kwenye mitandao kitu ambacho
nilijiuliza usiku huo huyo mpigapicha alikuwa wapi?”
SHAKA KUBWA YA DP
“Sisi DP, mashaka yetu makubwa ni
mazingira mazima ya namna kiongozi huyo alivyofariki dunia. Hata mtoto
hawezi kudanganywa kwa namna hiyo. DP ina taasisi ya kufanya uchunguzi
iitwayo Liberty International Foundation iliyokuwa ikisimamiwa na
marehemu. Ipo kazini kwa sasa ili kubaini ukweli wa kifo cha mwenyekiti
na tutaweka wazi kila kitu.”
“Laini pia tunaitaka serikali kufanya uchunguzi na kutoa taarifa hadharani.”
MWENYEKITI KIJIJI AIBUKA NA YAKE
Uwazi pia lilifika aneo la ajali na kujionea kwa macho mazingira yake na kupata maelezo kutoka kwa baadhi ya mashuhuda.
Joshua Mohamed Msigala ni Mwenyekiti wa
Kijiji cha Msolwa, Chalinze, Pwani palipotokea ajali. Yeye anasimulia
mambo aliyoelezwa na mmoja wa majeruhi, Mchungaji Patrick Mgaya siku ya
tukio.
“Kwanza kabisa waandishi wa habari
mmefanya vizuri kufika eneo la tukio na kujionea hali halisi. Nawaeleza
hali halisi ilivyokuwa mpaka mimi kufika eneo la ajali.
“Siku hiyo asubuhi ya saa kumi na moja
na nusu kama sikosei, nikiwa nyumbani nilipigiwa simu na dereva mmoja wa
lori anayenijua. Akasema ameona ajali maeneo yangu lakini hajui kama
kuna waliokufa au la!”
MWENYEKITI AWAHI NA BODABODA
“Kusikia hivyo, nilichukua bodaboda ili
niwahi. Nilifika ndani ya dakika kama kumi tangu kutokea kwa ajali.
Nilikuta mwili wa Mtikila umelala pembeni ya gari huku wengine watatu
waliodai walikuwa ndani ya gari wakiwa wamesimama tu.
“Ila kati ya hao watatu, mmoja alijitambulisha kuwa ni Mchungaji Mgaya, yeye wakati nafika alikuwa akiongea kwa simu.”
ALICHOAMBIWA NA MCHUNGAJI
“Nilimuuliza mchungaji ilikuwaje?
Akasema wakati wanapata ajali hiyo, marehemu Mtikila na wengine wawili
walichomoka ndani ya gari hali iliyosababisha kifo cha Mtikila. Hata
hivyo, kwa upande wangu sikuamini kama wote walichomoka kutoka kwenye
gari bali mazingira yalionesha walitoka wenyewe.
“Mchungaji alizidi kuniambia kuwa, gari
lilipaa juu zaidi ya futi kumi na kugonga mti kisha likapinduka na
kulalia paa (kwenye Uwazi siku ya tukio, mchungaji alisema gari
lilibiringika).
“Lakini pia siamini, kwani pamoja na
kuona alama katika mti sikubali kama zilisababishwa na ajali kwani kama
ni hivyo gari lingekuwa limepondeka zaidi juu lilikoangukia tofauti na
lilivyokuwa likionekana.”
KILICHOMSHANGAZA ZAIDI MWENYEKITI
Mwenyekiti huyo alizidi kusimulia
kushangaa kwake: “Kitu kingine kinachonishangaza ni kwamba, kwa maelezo
yao gari liliacha barabara likawa linaendeshwa pembeni kwa umbali wa
meta mia moja (urefu wa uwanja wa mpira). Kwa nini dereva asipunguze
mwendo ambapo angefanya hivyo gari lisingefika kwenye mti.”
“Kinachoshangaza kingine ni kwamba,
hakuna majeraha yaliyoonekana kwa macho kwa walionusurika hata kuonesha
kwamba walikatwa na vioo wakati wakirushwa nje kutoka ndani ya gari.
Hata viti vya mbele vilikuwa vilevile, havikuharibika na kama majeruhi
walirushwa nje walipitia wapi?”
WALIOFIKA AWALI
Mwenyekiti huyo alisema anawashukuru
askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kambi ya Kizuka
na Sangasanga waliokuwa wakipita ambapo walifika kutoa msaada.
“Baadaye mimi nilifanya mawasiliano na
Polisi wa Kituo cha Chalinze (Bagamoyo) ambapo walifika eneo la tukio.
Pia polisi wa mkoa nao walifika na saa 12:30 asubuhi majeruhi na mwili
wa marehemu walipelekwa Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi.”
Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha
Msolwa, Joseph Hamad kwa upande wake alisema alipokea taarifa saa 3
asubuhi na alipowasiliana na mwenyekiti alimwambia yupo katika eneo la
tukio.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho
waliohojiwa na Uwazi walisema wameshangazwa na ajali hiyo iliyosababisha
kifo cha Mchungaji Mtikila na kuitaka serikali kufanya uchunguzi wa
kina.
SIMU YA MTIKILA YAZUA UTATA
Mpaka tunakwenda mitamboni, familia ya
Mtikila ilisema, jana ilitarajia kufuatilia simu ya marehemu kwani
haijulikani ilipo na pia kujua walipo dereva (George Ponella) na
msaidizi wake (Ally Mohamed) ambapo awali, dereva alishikiliwa na jeshi
la polisi.
Chanzo: Global Publishers
0 comments:
Post a Comment