Wanafunzi wa Shule ya Arusha Sekondari wameiomba Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutafuta ufumbuzi kwa wanafunzi waliojiandikisha vituo
tofauti na walipo sasa ili waruhusiwe kupiga kura.
Waliyasema hayo wakati wa mafunzo ya elimu ya uraia na
mpigakura yaliyotolewa na Taasisi ya Dira ya Vijana Tanzania (TYVA) jana.
Katika mchango wake kuhusu elimu hiyo, mwanafunzi wa kidato
cha sita shuleni hapo, Glory Kamwela, aliiomba serikali kurekebisha kasoro za
uandikishaji zinazosababisha wanafunzi wa shule za bweni na taasisi za elimu ya
juu, kukosa haki ya kupiga kura kutokana na kujiandikisha maeneo tofauti na
wanayokuwapo siku ya kupiga kura.
Alisema kwa mfano wanafunzi wengi mwaka huu watakosa haki ya
kupiga kura kutokana na baadhi kujiandikisha maeneo tofauti na wanapokuwapo
siku ya kupiga kura.
“Serikali lazima
irekebishe hali hii kwa chaguzi zijazo,” alisema.
Kwa upande wake, Naylah Ally, anayesoma kidato cha sita,
alivitaka vyama vya siasa, wagombea na taasisi zinazohusika na utoaji wa elimu
ya uraia, upigaji kura na kunadi sera kuelekeza nguvu maeneo ya vijijini.
“Huko ndiko
wanakoishi wapigakura na wananchi wengi wanaokabiliwa na changamoto ya
mawasiliano na upatikanaji wa habari,” alisema.
Alisema kampeni na harakati nyingi za kisiasa na uchaguzi
hufanyika mijini ambako kuna mfumo rahisi wa mawasiliano huku maeneo ya
vijijini yakisahaulika au kutopewa kipaumbele.
Wanafunzi hao walisema somo la uraia linalofundishwa sasa
hivi shuleni lina upungufu wa mkazo wa eneo la muhimu la uzalendo, uadilifu na
uwajibikaji katika jamii.
Maafisa kutoka taasisi hiyo, Zulekha Ibrahim na Dianarose
Leonce, waliwataka wanafunzi na vijana wote wenye umri na sifa ya kupiga kura
kuchanganua hoja, sera na ahadi za wagombea na vyama.
Rais wa Serikali ya wanafunzi shuleni hapo, Innocent
Benjamin, alisema elimu ya uraia na uzalendo itawajengea vijana uwezo wa
kujitambua mapema.
0 comments:
Post a Comment