Masanja Mwinamila (44) mara baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega Juni 15, 2015.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Juma Bwire akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo Juni 16, 2015.
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Nzega leo hii imemhukumu Masanja Mwinamila
(44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya
Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora
kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kuteka mtoto mwenye albinism, Margreth
Hamisi (6).
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Saraphine Nsana, alitoa hukumu hiyo
baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka na kukiri kutenda kosa hilo.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo
Juni 15, 2015 majira ya saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Ugembe II, Kata
ya Mwakashanhala wilayani Nzega, mtuhumiwa alimteka binti huyo kwa
lengo la kwenda ‘kumuuza’ ili ajipatie fedha (kiasi kimehifadhiwa).
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi
inayohusisha utekaji nyara, kujeruhi na mauaji dhidi ya watu wenye
albinism kuchukua muda mfupi zaidi, kwani ndiyo kwanza kesi hiyo ya
Jinai Namba 116/2015 imefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na
kutolewa hukumu.
Mafanikio ya kukamatwa kwa Masanja
Mwinamila akiwa katika harakati za kutaka kumuuza mtoto Margreth Hamisi,
ambaye ni mpwa wake, yametokana na umakini wa Jeshi la Polisi nchini
ambapo maofisa wake wa Kikosi Kazi cha Taifa waliweka mtego na
kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa kabla hajamdhuru mateka wake.
Tukio hilo limefanikisha kuubomoa mtandao
hatari wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani ni
takriban wiki tatu tu tangu maofisa usalama walipofanikiwa kuwanasa watu
wengine sita wakiwa katika harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa
ya binadamu (albino) mjini Kahama Mei 22, 2015 ambapo tayari
wamekwishafikishwa mahakamani pamoja na wengine watatu waliokamatwa
baadaye.
Matukio hayo mawili makubwa yaliyotokea
katika kipindi hicho yamedhihirisha namna serikali kupitia jeshi hilo na
vyombo vingine vya usalama inavyoshughulikia mitandao hiyo hatari usiku
na mchana ili kuhakikisha Watanzania wote wanaishi kwa amani na
usalama.