Wananchi wa Kenya wameshangazwa na taarifa ya
mwanamume mmoja aliyezinduka akiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti
katika hospitali moja mjini Naivasha umbali wa kilomita tisini kutoka
mji mkuu Nairobi.
Mwanamume huyo Paul Mburu mwenye umri wa miaka
24, alipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kunywa sumu kwa lengo
la kujitoa uhai,kutokana na ugomvi wa kinyumbani na babake ingawa
alisemekana kufariki Jumatano usiku wakati akipokea matibabu.
Wafanyakazi wa hospitali hiyo
walipigwa na butwaa na hata kutoroka walipoona mwili wa mtu waliyedhani
ni maiti ukisonga na kuonyesha dalili za kuwa hai katika chumba cha
kuhifadhia maiti.
Afisaa mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo ya
wilaya, Dokta Joseph Mburu, alisema kuwa dawa iliyotumiwa kumtibu Mburu
hufanya moyo kupiga polepole hali ambayo huenda ilimfanya muuguzi
kudhani kuwa mgonjwa alikua amefariki.
Mwanamume huyo alisikika akimtaka mmoja wa
wafanyakazi katika chumba cha kuhifadhia maiti kumsaidia kwani alikuwa
anahisi baridi kali na hapo ndipo mmoja wa wafanyakazi alipotimua mbio
kwa hofu.
Nusura Mburu awekwe kwenye jokovu la kuhifadhia maiti.
Jamaa za mwanamume huyo akiwemo babake walikuwa
wametembelea chumba cha maiti siku ya Alhamisi ili kujiandaa kwa mazishi
, lakini baadaye mchana walifahamishwa kuwa Mburu alikuwa hai.
Souce: BBC Swahil
0 comments:
Post a Comment