Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa
zilizoanza kunyesha jana alfajiri na kusababisha maafa makubwa yakiwamo
kuharibiwa kwa makazi ya watu, majengo ya Serikali zikiwamo shule, vyuo
na mahakama.
Habari zinasema mafuriko hayo pia yalichangiwa na
mvua kubwa iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia jana katika sehemu za
milima iliyopo Kilosa na Mvomero, hivyo Mto Mkundi kushindwa kuhimili
maji hayo.
Mashuhuda walisema waliona maiti ya mtu ikielea
kwenye maji yaliyokuwa yakipita kwa kasi, tukio ambalo lilithibitishwa
na Diwani wa Kata ya Magole, Juma Rajabu Chewe. Chewe alisema maiti hiyo
ilionekana ikielea eneo la Mateteni na kwamba taarifa zilitolewa polisi
ili aopolewe. Hadi jana jioni idadi ya watu walioathiriwa na maafa
ilikuwa bado haijafahamika.
Maji yasambaa kwenye vijiji mbalimbali
vinavyozunguka mto huo na kuwalazimisha baadhi ya watu kulazimika
kujiokoa kwa kupanda kwenye paa za nyumba zao huku wengine wakikwea juu
ya miti.
Baadhi ya watu walikutwa na mafuriko hayo
mashambani na walipozidiwa na nguvu ya maji walijiokoa kwa kushikilia
vitu mbalimbali ikiwamo miti, huku baadhi yao wakipoteza nguo walizokuwa
wamevaa walipokuwa kwenye harakati za kujiokoa.
Polisi waliofika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji
walilazimika kuomba helikopta kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar es
Salaam ili kuwaokoa watu waliokuwa kwenye paa za nyumba na kwenye miti
iliyokuwa imezungukwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alitaka
kuwapo kwa uvumilivu wakati Serikali ikiendelea na taratibu za kuwaokoa
walioko juu ya miti na kutoa misaada kwa walioathirika.
Alisema kuwa kutokana na hali kuwa mbaya, ofisi
yake ililazimika kuomba helikopta kwa ajili ya kuongeza nguvu ya juhudi
za uokoaji.
Taharuki kubwa
Mafuriko hayo yalizua taharuki kubwa kiasi cha
wananchi kutawanyika ovyo wakiwa hawajui cha kufanya, kutokana na nyumba
zao kuharibiwa na mali zao hususan mazao yakisombwa na maji.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kina mama wakiwa na
watoto ambao walionekana katika makundi wakiomba msaada baada ya
kukimbia makazi yao, huku wengi wakiwa wamelowa kutokana na kunyeshewa.
Mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Zahra Maulid alisema
wanapata taabu na watoto kwani hawajui watakula nini baada ya mazao yao
ukiwamo mpunga, mahindi na alizeti kusombwa na maji.
“Hapa hata hatujui tutaishi vipi maana vyakula
vyetu vyote vimesombwa na maji, tunachoomba Serikali itupatie msaada wa
haraka na mpaka sasa hatujui mlo wetu wa leo na hata wengine hawana
makazi,”alisema Zahra.
Habari zaidi kutoka Dumila zilisema, madarasa ya
Shule ya Msingi Magole, nayo yalifunikwa na maji na wanafunzi
waliokuwamo walijiokoa kupita madirishani.
Majengo ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Dakawa,
Chuo cha Veta Dakawa na Mahakama ya Mwanzo Dakawa nayo yaliharibiwa na
mafuriko hayo.
Wanafunzi wa Sekondari ya Dakawa walikuwa nje ya
mabweni wakisubiri maji kukauka. Majalada ya kesi mbalimbali katika
Mahakama ya Mwanzo Dumila yalilowa maji, huku tope zito likionekana
ndani ya chumba cha mahakama hiyo.
Mafuriko hayo pia yalisababisha kusombwa kwa nguzo
za umeme na kufungwa kwa barabara nyingine kadhaa kutokana na miti
mikubwa kukatika na kutanda katika barabarani hizo.
Pia vituo 11 vya treni vilivyoko mkoani Morogoro vimeathirika kutokana na mafuriko baada ya kusombwa na maji.
Magari yakwama
Magari zaidi ya 5,000 yaliyokuwa yakitokea Dar es
Salaam, Tanga na Pwani kuelekea Bara na yale yaliyokuwa yakitokea Bara
kwenda Dar es Salaam yalikwama huku, mengine yakigeuza na kurejea
yalikotoka.
Abiria aliyekuwa katika moja ya mabasi
yaliyokwama, Godfrey Wambura alilalamikia kukosekana kwa huduma za
kijamii katika eneo hilo na kwamba bidhaa muhimu zilikuwa zimeanza
kuuzwa kwa bei ghali. Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ambaye
alifika mapema kwenye eneo hilo, alishauri magari yaliyotokea yanatokea
upande wa barabara kurudi Dodoma na kwenda Iringa kwa ajili ya kuja Dar
es Salaam.
Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) wa Mkoa wa
Morogoro, Doroth Mtanga alisema haifahamiki ni hasara gani iliyotokana
na kuvunjika kwa daraja hilo.
Wakati huohuo, jana Serikali ilitangaza kufunga
Barabara ya Morogoro – Dodoma kuanzia jana, na kuwashauri wale wenye
safari za lazima kutumia barabara mbadala kwani eneo la Dumila
halipitiki.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge,
William Lukuvi aliliambia gazeti hili jana jioni kuwa: “Magari
yanayoendelea kutumia barabara hiyo yanaweza kusababisha maafa zaidi
maana eneo hilo halipitiki, lakini kibaya zaidi Kijiji cha Dumila ni
kidogo, hakiwezi kuhimili idadi ya watu wote waliokwama na
watakaokwama.”
Aliongeza: “Magari yanayotoka Dar es Salaam
yapitie Chalinze – Arusha – Babati - Singida – Mwanza na yale yanayotoka
Mbeya yatumie Barabara ya Iringa – Dodoma – Arusha – Kondoa kuelekea
Arusha au Mwanza.”
Alisema mafundi wameanza kazi ya kurejesha hali ya
kawaida katika daraja lililobomoka na kwamba barabara hiyo imefungwa
kuanzia jana na itaendelea kufungwa leo, huku akiwashauri madereva wa
magari yaliyoko katika eneo hilo waondoke na kurejea yalikotoka.
Kuhusu waliopatwa na maafa, waziri huyo alisema
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa
Mkoa, Joel Bendera ilikuwa eneo la tukio kufanya tathmini ya maafa hayo.
“Hapa kwetu tumekusanya mahitaji ya chakula,
mablanketi, mahema na vyote hivyo vinaondoka jioni hii (jana) kwa gari
la jeshi kwenda eneo la maafa,” alisema Lukuvi.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment