Dar es Salaam : Mabadiliko yaliyofaywa na Rais Jakaya Kikwete
katika Baraza la Mawaziri, yamewaokoa baadhi ya mawaziri ambao walitajwa
na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wabunge kuwa ni
‘mizigo’ na kwamba walipaswa kung’oka.
CCM kupitia kwa sekretarieti yake ikiongozwa na
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana iliwataja baadhi ya mawaziri kuwa ni
mizigo, baada ya kubaini udhaifu katika utendaji wao hivyo kusababisha
malalamiko kutoka kwa wananchi wakati viongozi hao walipofanya ziara
katika baadhi ya mikoa.
Baadhi ya mawaziri hao walihojiwa na Kamati Kuu ya
CCM ambayo baada ya kukamilisha kazi yake iliwakabidhi kwa Rais Kikwete
ili aweze kuchukua hatua.
Kadhalika, katika mkutano wa 11 wa Bunge
uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana, orodha ya mawaziri mizigo
iliongezeka baada ya wabunge kuwachachamalia baadhi yao baada ya
kutoridhishwa na utendaji wao.
Mawaziri hao ni pamoja na Christopher Chiza
(Kilimo, Chakula na Ushirika), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru Kawambwa, aliyekuwa naibu wake, Adam Malima, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Manaibu wake; Aggrey
Mwanri na Kassim Majaliwa.
Kati yao aliyehamishwa ni Malima pekee ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha, huku wengine wakibaki katika nafasi zao.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana,
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema, Rais anapofanya uteuzi
huzingatia vigezo vingi.
“Unaposema mawaziri mizigo inategemea maana,
inawezekana kabisa kukwama kwa utendaji katika wizara husika
hakumhusishi waziri moja kwa moja, kwa hiyo Rais anaangalia sababu za
kukwama ni zipi, kimsingi yapo mambo mengi,” alisema Balozi Sefue na
kuongeza: “Mfano upatikanaji wa fedha ukiwa ni tatizo, huwezi kumlaumu
waziri husika moja kwa moja, pia katika masuala ya fedha, huwezi
kumtwisha mzigo waziri wa fedha maana inawezekana kabisa kwamba wakati
huo makusanyo ya mapato siyo mazuri.”
Alisema hakuna wizara isiyokuwa na matatizo, hivyo
siyo sahihi kumbebesha lawama waziri binafsi kwa matatizo ambayo msingi
wake siyo usimamizi.
Kuhusu Dk Kawambwa na Ghasia, Katibu Mkuu Kiongozi
alisema: “Inawezekana Rais ameamua kuwaacha waendelee kwa sababu tayari
wameanza kuchukua hatua kuyakabili matatizo yaliyopo, maana hapo
inakuwa bora zaidi kuliko kumteua mtu ambaye ataanza upya.”
Lugola, Mrema waponda
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola ameponda
mabadiliko katika Baraza la Mawaziri akisema hakuna jipya
litakalojitokeza baada ya kumwacha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na
mawaziri watatu katika Wizara ya Kilimo, Elimu na Tamisemi.
“Hata kama yeye Rais ndiyo mwenye mamlaka lakini wabunge,
wananchi na hata katibu mkuu wa chama waliona kuwa viongozi hao ni
mizigo, siamini kama kulikuwa hakuna viongozi wengine mbadala,” alisema
Lugola na kuongeza: Kama sura kubwa ya baraza ni ileile na Waziri Mkuu
ambaye ni injini ameachwa tutegemee nini?” alihoji Lugola.
Aliongeza; “Pinda alitakiwa kupumzishwa kwa sababu
amekuwa mpole, Rais alitakiwa kupangua kuanzia juu,” alisema.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema viongozi wa CCM wanapaswa
kujifunza kutokana na Rais Kikwete ‘kuwafungia masikio’ kwa
kutowawajibisha mawaziri walioitwa ni ‘mizigo.’
Mrema aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
alisema fundisho ambalo wanapaswa kulichukua ni kuacha kuzungumza mambo
yanayowahusu viongozi wao hadharani, bali watumie vikao.
“CCM wajifunze kujisahihisha kwenye vikao vyao.
Huoni sasa hii ni aibu? Maana walipiga kelele hadharani, matokeo yake
Rais (Kikwete) hakukubaliana nao,” alisema Mrema. Kiongozi huyo ambaye
ni Mbunge wa Vunjo, alisema mabadiliko yaliyofanywa katika Baraza la
Mawaziri yataleta tija iwapo watawajibika ipasavyo.
Mrema alisema utendaji wa mawaziri wengi mara
nyingi ni wa mazoea, hakuna ubunifu, jambo ambalo halitoi changamoto ya
kiutendaji.
Mkazi wa Kiteto, Alayce Bajuka alisema: “Hawa
waliokuwa wanaitwa mizigo hata chama tawala kiliwalalamikia nashangaa
wamerudi wote tena bila kubadilishwa wizara.”
Chanzo: mwananchi
0 comments:
Post a Comment