WAHANGA wa mafuriko katika Manispaa ya Tabora wamekabidhiwa msaada
wa chakula tani 1.4 za unga wenye thamani ya zaidi ya sh milioni 1.2
baada ya nyumba zao kubomoka kutokana na mvua kubwa zinazonyesha.
Msaada huo ulitolewa na uongozi wa Manispaa ya Tabora kwa wahanga hao zaidi ya 100.
Akikabidhi msaada huo wa chakula kwa uongozi wa Kata ya Malolo katika
manispaa hiyo ili kuzigawia familia 102 zinazoishi Mtaa wa Uzunguni,
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Suleiman Kumchaya, aliwahakikishia wananchi
hao kuwa serikali ipo pamoja nao na itafanya kila linalowezekana
kukabiliana na hali hiyo.
Alisema maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo yako bondeni ndiyo
maana ikinyesha mvua kubwa maji kutoka maeneo mbalimbali hufurika
katika maeneo hayo kwa kukosa mahala pa kutokea.
“Ndugu zangu nawapeni pole kwa matatizo haya, lakini napenda
kuwahakikishia serikali iko pamoja nanyi na tutafanya kila liwezekanalo
kumaliza matatizo haya na kwa kuanzia nimemwagiza meneja wa Tanroads
alifanyie kazi,” alisema.
Aidha, aliwataka wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada
zinazofanywa na uongozi wa manispaa hiyo kuwasaidia wahanga hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Alfred Luanda, alisema
watahakikisha kila mmoja aliyeathirika na mafuriko hayo anapata msaada
unaostahili.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage naye alitembelea wahanga hao na kuwapa pole.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment