LATEST POSTS

Saturday, January 4, 2014

CCM yamtolea uvivu Lowassa Urais 2015

Dar es Salaam. Unaweza kusema sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula kusema kuwa wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015 watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini;
“Wapo watu wanataka waichanechane CCM kwa sababu ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata urais. Kuna makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe hatuwezi kuyafumbia macho.”
Akifafanua hilo Mangula alisema: “Tutawaita wote walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwanini wanafanya hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza katika mikutano wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua dhamira yao ni nini.”
Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kusema mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya Lowassa siku mbili zilizopita, kutangaza nia ‘kimtindo'.
akisema anaanza rasmi safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Mangula aliwashukia vigogo wa chama hicho wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati ya Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa salamu za mwaka mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.
Ataja kanuni za uongozi
Katika mkutano huo Mangula alisaidiwa kusoma kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa CCM na wanachama taifa, Masoud Mbengula.
Moja ya kanuni hizo inasema “Ni mwiko kwa kiongozi wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au eneo analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye mwenyewe ama mgombea anayemuunga mkono.”
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa msaliti na hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza chama wakati wowote.
“Tutawachukulia hatua kali wale wote ambao wameanza kuonyesha dalili kama hizo za kutoa michango, misaada, zawadi. Lengo la mwanachama huyo ni kutaka kuungwa mkono, wanaotaka madaraka wasubiri muda ufike ndiyo wafanye hivyo.”
Aliongeza “Hivi haya mapenzi ya kusaidia yameanza lini, fedha hizo zinatoka wapi, hawa wanaosadiwa wanatakiwa kutambua kuwa yote hayo ni kampeni kwa kuwekeza, hatuwezi kuwa na viongozi wa nchi wa namna hii wa uchu wa madaraka, CCM haitawafumbia macho lazima kanuni na miongozo ifuatwe.”
“Kuna watu wameanza kudhani kuwa muda wa kampeni umeanza, muda wa kampeni haujafika na hakuna majina yaliyotangazwa ya kugombea udiwani, ubunge hata urais,” alisema Mangula na kuongeza;
“Kuna makundi yanaifanya nchi ya Somalia isitawalike. Makundi ya aina hiyo naona yapo hata CCM; watu wanaibua vita ya maneno ndani ya chama, wanataka wakichanechane chama kwa sababu ya uroho wa madaraka tu.”
Bila kuyataja makundi hayo Mangula alisema: “Utaongozaje nchi ambayo imegawanyika katika makundi? Watu wameanza kuvuruga chama chetu, kila mtu ana kundi lake na wakati mwingine wanayatumia makundi kuwabomoa wenzao, hili jambo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo.”
Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Makamba hivi karibuni amekuwa akitoa misaada kwa vikundi vya waendesha bodaboda katika mikoa mbalimbali, hali ambayo inatafsiriwa kuwa ni kujiimarisha kisiasa.
Hata hivyo, mwaka jana Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa alinukuliwa akisema kuwa sio vibaya kwa wanachama wa chama hicho kuonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama, lakini siyo kufanya kampeni.
Mei 26 mwaka jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Iringa, alisisitiza kwamba chama kitamwadhibu bila huruma mwanachama yeyote anayejipitisha katika maeneo mbalimbali na kufanya kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.
Akifunga mafunzo ya makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa mjini Dodoma mwaka jana, Rais Kikwete alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama bunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.
Uchaguzi Serikali za Mitaa
Mangula akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu alisema, viongozi wote wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Vitendo vya rushwa ndio vilitufanya katika chaguzi zilizopita kufanya vibaya, watu walinunuliwa kadi, sasa viongozi wa matawi wawe makini tusirudi tulikotoka na tukibaini mtu hafuati kanuni tutamwajibisha,” alisema Mangula.
Chanzo: Mwanchi


0 comments: