KATIKA Gazeti la Ijumaa Wikienda la juzi Jumatatu, Toleo Namba 354 ukurasa wake wa mbele kuna habari yenye kichwa kisemacho; MBONGO ABAKWA CHINA, AFA!
Katika habari hiyo, kulisindikizwa na vichwa vidogo vilivyosomeka; Wabakaji ni Wanigeria watano, maiti yake yakutwa haina figo, moyo!
Habari hiyo ilimhusu Mtanzania aliyejulikana kwa jina la Sabrina au Habiba kwamba, aliondoka Bongo kwenda Guangzhou, China akidanganywa na mwanamke mmoja kwamba anakwenda kufanya kazi kwenye saluni ya kike.
Habari zilisema baada ya kufika China, mwanamke huyo alimnyang’anya Habiba hati ya kusafiria na kumwingiza kwenye biashara ya ukahaba kwa kumuuza kwa wanaume huku ujira akiuchukua yeye.
Ilidaiwa kuwa, tabia hiyo ndiyo iliyopo kwa sasa kwamba, kuna wasichana wanachukuliwa kupelekwa nchini humo kwa kudanganywa kufanya kazi saluni matokeo yake huishia kwenye ukahaba.
NDUGU WASOMA GAZETI, WAJITOKEZA
Sasa, baada ya gazeti hilo kuingia mtaani siku hiyo, mazito yakaibuka.
Ndugu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni kaka wa marehemu alimpigia simu Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa ya Global Publishers, Oscar Ndauka na kumweleza kuwa wamesoma habari za kifo cha Habiba kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.
Akizungumza kwa sauti iliyojaa simanzi, ndugu huyo alisema nyumbani kwao ni Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam.
Mhariri: Ndugu poleni sana! Je, naweza kutuma waandishi wangu wakafika hapo na kujua mawili matatu kuhusu marehemu?
Ndugu: Hamna tatizo, baba yupo ila mama alikuwa Vikindu (Dar) ndiyo anakuja yuko njiani.
Mhariri alituma waandishi wawili kufuatilia mkasa huo ambao umewatikisa Wabongo waishio eneo la Guangzhou nchini China.
WAANDISHI MSIBANI, WAKUTANA NA BABA MZAZI
Akizungumza msibani, baba mzazi wa marehemu, mzee Yusuf Ally alisema Habiba aliondoka nchini kwa kutoroka kwenye Sikukuu ya Idd El Haj mwaka 2012.
Alisema hakuwa na mawasiliano mazuri na bintiye huyo si kwa sababu ya kutoroka tu bali kwa vitendo alivyokuwa akivifanya na kila alipomuonya binti huyo hakusikia, mwishowe akaamua kukata mawasiliano naye.
“Sikuwa na mawasiliano na Habiba tangu Machi 2010 kwani aliniudhi sana,” alisema mzee huyo licha ya kwamba alikuwa akiporomosha machozi kufuatia taarifa za kifo cha binti yake.
NINI HASA UGOMVI WA HABIBA NA BABA YAKE?
Akiendelea kusimulia maisha aliyokuwa akiishi na mwanaye huyo, mzee Yusuf alisema:
“Habiba alibadilika tabia akawa hataki kusoma. Mbaya zaidi kilichonikera ni pale alipokataa kwenda kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2010. Kiukweli iliniuma sana.
“Nilimsomesha kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, nilikuwa najinyima kula kwa ajili yake, siku ya mtihani akakataa kwenda shule, niliumia sana hasa nikikumbuka fedha zangu nilizotupa kwa ajili yake,” alisema.
JINSI ALIVYOONDOKA BONGO
Naye dada wa Habiba, Aziza Said ambaye alikuwa akiishi na marehemu alisema kwamba ilikuwa siku ya Idd El Haj mwaka 2012 ndiyo siku ambayo mdogo wake huyo alitoroka nyumbani na kwenda kujificha kusikojulikana.
“Siku hiyo nilimwachia fedha ili aende saluni akamsuke mtoto, mi nikaenda Kariakoo. Niliporudi nikakuta fedha za kusukia ziko mezani na mtoto anacheza nje.
“Nilimuuliza mwanangu mama mdogo yuko wapi? Akanijibu hajui. Sikuwa na wasiwasi kwani nilijua alikwenda kwa mashoga zake kula sikukuu, kwangu alihisi ningembana. Kumbe mwenzangu yuko katika mipango ya kutoroshwa nchini,” alisema dada huyo na kuangua kilio.
MWANAMKE ALIYEMTOROSHA WANAMJUA
Familia hiyo ilisema mwanamke aliyemtorosha Habiba kutoka Bongo kwenda China wanamjua (jina tunalo) kwani waliwahi kuishi naye nyumba moja, Manzese jijini Dar lakini wakawa hawaongei naye kwa sababu ya tabia zake mbaya.
Walisema mwanamke huyo alianza kumbadili tabia Habiba miezi michache kabla ya safari ya China, hasa kwa mavazi ya ajabu na tabia ya kutotulia nyumbani.
Waliendelea kusema kuwa, ilifika mahali kutokana na tabia yake mpya isiyo na maadili, waliamini binti huyo ametumbukia kwenye mambo ya kigodoro (ngoma za uswahilini).
MARA YA MWISHO KUONEKANA WHATSAPP
Kaka wa marehemu Mohammed Yusuf Ally alipoongea na gazeti hili msibani hapo alisema kuwa mara ya mwisho kufanya mawasiliano na marehemu ilikuwa Valentine’s Day (Sikukuu ya Wapendanao) – Februari 14, mwaka huu, ambapo alimtumia ujumbe mfupi wa maneno katika Mtandao wa Kijamii wa WhatsApp lakini meseji hiyo haikujibiwa.
“Nimeshtuka sana leo kupata taarifa kwamba mdogo wangu amefariki dunia tena baada ya kusoma gazeti (Ijumaa Wikienda) huku kifo chake kikiwa cha kikatili kiasi hicho,” alisema akilia kaka huyo.
NYONGEZA NYINGINE YA TAARIFA
Kwa mujibu wa ndugu, mbali na miongoni mwao kulisoma Gazeti la Ijumaa Wikienda na kupata taarifa, lakini kwa mzee Yusuf habari zilimfikia baada ya jirani kununua gazeti hilo na kumpelekea nyumbani hapo.
KAKA AISHUKURU GLOBAL
“Nalishukuru hili gazeti (Wikienda) kwani bila ya wao kuandika tusingejua nini kinaendelea huko China,” alisema kaka wa marehemu huku akiwa ameshika gazeti hilo.
0 comments:
Post a Comment