SHAHIDI wa 20 katika kesi ya utoroshwaji wanyama aina ya twiga kwenda Uarabuni, Bw. Robert Nyanda amesema pamoja na gari aina ya Fuso iliyobeba wanyama hao, kulikuwa na kundi kubwa la vijana waliosaidia upakuaji, upakiaji maboksi yenye wanyama hao.
Alisema siku ya tukio, alimwona mshtakiwa wa kwanza, Kamran Ahmed na watu wengine waliokuwa kwenye gari ndogo wakiwa katika harakati za kusafirisha wanyama hao kwenda Qatar.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi, Simon Kobelo, shahidi huyo alidai mshtakiwa huyo alikuwa na watu wengine ambao walikwenda na gari ndogo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akiongozwa na wakili wa Serikali, Evetha Mushi, shahidi huyo kutoka Kampuni ya Swissport kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, alisema awali alikuwa akifanya kazi KIA.
"Siku hiyo nilikuwa uwanjani KIA, nilimwona mshtakiwa wa kwanza na watu wengine katika gari dogo, lakini pia kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa katika Fuso ambao walikuwa wakisaidiana kupima na kupakia mizigo katika ndege ya Qatar.
"Mimi nilikuwa na jukumu la kusimamia upakiaji mizigo katika ndege kwa maelekezo ya bosi wangu, Rosemary Israel, aliyenitaka niandae vifaa vya aina tatu kubebea vitu vizito," alisema.
Alisema wakati akiandaa vifaa hivyo, alifika uwanjani na kukuta gari aina ya Fuso likiwa karibu na Ndege ya Qatar, ambapo vijana waliokuwa wakisaidia upimaji wa mizigo.
"Baada ya mzigo kufika usiku wa manane, tulishirikiana na vijana waliokuwa katika gari la mizigo kuipakia kwenye ndege...Uwanja wa KIA una Kampuni ya Equity na TanzaniteOne ambazo hufanya kazi ya upakiaji mizigo kama wafanyavyo Swissport.
"Siku ya tukio Equity ndiyo walipokea ndege hiyo na kukodisha vifaa Swissport," alisema shahidi huyo.
Kwa upande wake, shahidi wa 21, Rewald Amani aliyekuwa Meneja Mwongozaji wa Ndege katika uwanja huo, alidai ndege hiyo ilitua nchini Novemba 24, 2010 katika kiwanja hicho na kuondoka Novemba 26, 2010 ikiwa salama kwenda Doha, Qatar.
Kesi hiyo itaendelea tena leo ambapo upande wa mashtaka utendelea kuleta mashahidi wake.
0 comments:
Post a Comment