LATEST POSTS

Thursday, March 13, 2014

Hatimaye ni Sitta achaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge la Katiba

WAJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba wamemchagua kwa kura za kishindo, Samuel Sitta, kuwa Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo.
Sitta alichaguliwa jana jioni na wabunge hao mjini Dodoma, ambapo alipata kura 487 dhidi ya Hashim Rungwe aliyepata kura 69 sawa na asilimia 12.3.
Akitangaza matokeo hayo Msimamizi wa Uchaguzi huo, Thomas Kashilila, alisema wajumbe waliopiga kura ni 563 na kura zilizoharibika ni saba.
Kashilila alimtangaza Sitta kuwa mshindi wa nafasi hiyo. Akishukuru baada ya kutangazwa mshindi, Sitta aliahidi wajumbe hao utumishi wa kasi, uzalendo, viwango na uadilifu.
Aliwapongeza wajumbe kwa kumchagua na chama chake CCM kumpitisha kwa kufanya mchujo wa haki na kwamba watu waliokuwa wakisema vibaya kwamba ana uhasama na Andrew Chenge, hawajui lolote kuhusiana na uhusiano wao.
Alisema yeye ndiye aliyempendekeza Chenge kwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Felix Mrema, kuwa naibu wake.
“Msiojua mnaweza kusema mambo mengi lakini kwenye kampeni kunakuwa na mambo mengi ndiyo maana wakati mwingine wanasema wapambe nuksi,” alisema Sitta.
Aliahidi kuandaa hotuba ya shukrani kwa watu wote wakiwemo wale waliokuwemo kwenye timu yake ya kampeni kwani kwa sasa bado alikuwa haamini. Alisema akishaapishwa ataeleza mikasa yote iliyotokea usiku na mchana wakati wa kampeni.
Kwa upande wake, Rungwe, alikubali matokeo hayo ambapo alimpongeza Sitta kwa kuibuka mshindi.
Awali, akijieleza wakati wa kuomba kura Sitta, alisema aliahidi kuendesha Bunge hilo kwa viwango na kasi pasipo kupendelea upande wowote na kwamba atatenda haki.
Sitta aliongeza kuwa ana uzoefu wa kutosha kwani amekuwa mbunge kwa miaka 29,Waziri kwa awamu zote nne kwa miaka 14 na Spika wa Bunge la 9 ambalo lilikuwa ni Bunge la viwango.
Alisema wajumbe kumchagua na kumweka kwenye kiti hicho ni sawa na kumrudisha chura kwenye maji aliyoyazoea, kwani lazima ataogelea tu.
Sitta alisema siku zote yeye ni mtu wa kujipanga, hivyo aliwataka wajumbe pamoja na Watanzania wategemee kupata Katiba bora na yenye viwango vinavyokubalika.
"Nitasimamia kanuni bila kumpendelea mtu wala upande wowote kwa kuwa mtetezi hodari wa haki ambayo itawawezesha wajumbe kuishi vizuri mjini Dodoma," alisema huku akishangiliwa na wajumbe hao.
Mara baada ya kujieleza mjumbe wa Bunge hilo, Kangi Lugola, alitaka kujua anakuwa na maana gani anaposema amejipanga kuendesha Bunge hilo kwa viwango na kasi?.
Akijibu swali hilo, Sitta alijibu kuwa viwango na kasi ni falsafa yake ya kufanya kazi hivyo wananchi waelewe kuwa watapata Katiba bora na yenye viwango.
Kwa upande wake, David Silinde, alitaka kujua Sitta atachukua hatua gani kama Bunge litafikia hatua ya kutoelewana na kutishia kuvunjika, Sitta alisema Mwenyezi Mungu atupilie mbali jambo kama hilo kwani Watanzania hawatarajii Bunge livunjike.
Alisema kwenye Bunge hilo kuna watu wenye busara na hekima na Rais hakufanya makosa kuchagua watu hawa. "Tumesikia wapo watu watatu, wanne nitashughulika na hao watu wanaotaka Muungano uvunjike kwani wanajua maoni yangu kuhusu Muungano ndiyo maana wamenizushia kuwa nimelazwa hospitali nipo mahututi," alisema na kuongeza kuwa yupo fiti na imara.
Mara baada ya Sitta kujieleza na kurejea katika nafasi alipewa mkono wa pongezi Waziri Mkuu aliyejiuzulu wadhifa huo, Edward Lowassa, kwa sakata la Richmond wakati Sitta akiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa upande wake, Rungwe, aliwaomba wajumbe kumchagua kwani ana uzoefu wa kutosha katika mambo mbalimbali ya kisheria akiwa ni wakili wa kujitegemea.
Rungwe alisema ana uwezo wa kuongoza Bunge hilo kwani hakuna chuo ambacho kinafundisha namna ya kuongoza Bunge hilo.
Alisema yeye ndiye alikuwa Mwafrika wa kwanza kufanya biashara ya kuuza magari hapa nchini.

0 comments: