LATEST POSTS

Monday, April 14, 2014

Bomu latupwa baa Arusha, lajeruhi

Watu kadhaa wamejeruhiwa kutokana na mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu katika baa maarufu ya Arusha Night Park katika eneo la Mianzini katika jiji la Arusha.
Tukio hilo lilitokea jana saa mbili usiku wakati mamia ya watu wakiwa katika baa hiyo wakiangalia  mechi ya soka ya Ligi Kuu ya England kati ya Chelsea na Swansea. Chelsea ilishinda 1-0.
Mmoja wa wamiliki wa baa hiyo, Angelo Mwoleka pia alithibitisha kutokea mlipuko huo na kueleza kujeruhiwa watu kadhaa.
“Ni kweli kuna mlipuko umetoka na watu kujeruhiwa, mimi sikuwepo ila nipo njiani nakwenda eneo la tukio, “alisema.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lymo alisema watu saba waliumia vibaya kutokana na bomu hilo na walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa Arusha ya Mount Meru.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus (pichani), alisema: “Hivi sasa tunaendelea na uokoaji na uchunguzi umeanza.”
Tukio hilo limekuja wakati bado jiji la Arusha likiwa na kumbukumbu ya kushambuliwa kwa mabomu kwa Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo eneo la Olasiti  na jingine Uwanja wa Soweto wakati Chadema walipokuwa wakifunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani. Katika matukio yote hayo, watu sita waliuawa na wengi kujeruhiwa.

Hali ya sintofahamu iliyowakumba wakazi wa jiji la Arusha baada ya bomu kulipuka jana.
Majeruhi baada ya bomu kulipuka.
Kijana ambaye hakufahamika jina lake baada ya kupata majeraha makubwa mguuni.
Mmoja wa maeruhi akiwa hoi baada ya mlipuko.

0 comments: