Leo tuangalie habari tatu zinazokabana kabali na maisha yetu
magumu Waafrika. Ingawa ni za kuchoma moyo zitatupa azma ya kujaribu
kujua nini hasa chanzo cha adha zetu na kutafuta ufumbuzi.
Mosi ni kisa cha kina dada wa Kitanzania
wanaoendelea kukumbwa na hali za hatari sana baada ya kuahidiwa maisha
bora kule China. Kwamba wangepewa kazi za kulipwa mishahara minono
wayaboreshe maisha yao Bongo lakini wameishia gizani.
Giza totoro kiasi ambacho inadaiwa mmoja wao,
Habiba Yusuf Ali Abdallah, aliuawa karibuni. Habiba alibakwa, akapigwa,
figo yake ikanyofolewa kisha akarushwa mithili ya inzi toka ghorofani.
Ukweli wa madai haya umethibitishwa na dada mmoja
aliyeshuhudia maiti na kero ikamzonga kiasi cha kujitolea kuzungumzia
hatima ya wanawake vijana wanaokutwa na majanga nchini China.
Kwa woga wala jina hakuthubutu kulitaja.
Kazungumzia kupitia blogu ya Mtanzania,Jestina George hapa London wiki
mbili zilizopita.
Kisa nini?
Maisha magumu. Elimu duni. Ukosefu wa ajira...
Wanawake vijana wanaahidiwa ajira katika saluni,
maana wanaifahamu sanaa ya nywele au kazi za dukani. Hughilibiwa na
wanawake wenzao wa makamo waliokwishaishi China sasa wamepanga njama na
midume toka Nigeria. Wanigeria ni kama washawajulia dada zetu. Wakiwaona
ni kipepeo kuliona ua lenye asali. Na wanawake wa Kitanzania (hasa
ughaibuni) wakionjeshwa maneno mazuri na vipesa vya uongo na kweli,
hulegea na kulaghaika. Nauli za ndege chee, wanapofika China wanakuta
ibilisi.
Pasi zinachukuliwa kusudi wasitoroke. Vitisho.
Iliyobaki kulazimishwa kufanya ukahaba. Wanaokataa, madai yanaendelea,
huletewa hawa washashi wa Kinigeria (waliokubuhu ukuwadi na maisha
ughaibuni) huwabaka, huwapiga na baadhi kama Habiba kutolewa roho.
Labda tutadhani ni jambo geni maana hii ni mara ya
kwanza kusikia limewakumba Watanzania. Mwaka jana mwanabloga wa Kenya
anayeandika masuala ya safari kwa Kiingereza(“The African
Traveller”)alieleza namna ambavyo wanawake wa Kenya, Uganda, Afrika
Kusini, Ulaya na Bara Asia wanavyofanyiwa uanaharamu Bara Asia. Bloga
Msafiri anatujuza kisa cha dada wa Kiganda aliyejirusha toka ghorofa ya
nne mji wa Taman Kosas, Malaysia, akajiua.
Dada aliishi maisha ya kufungiwa, kupigwa na
kulazimishwa kulala mkuku na wanaume. Anasema wanawake hawa
hushurutishwa huo umalaya ili “kulipia” nauli ya dola 20,000.
Inapomalizika, siku za viza nazo zimekwisha,
hawana njia, ila kubaki na pasipoti zimefichwa. Kazi ya ngono usiku
mmoja ina rutuba ya dola 400 -mshahara wa mwezi saluni. Tamaa hii ya
kipato cha haraka huishia puani.
“Wanawake wa Kiafrika huwa mateka wa biashara ya ngono. Kwa
nini?” Anauliza Bloga Msafiri. “Nchi nyingi za Kiafrika ni maskini na
wengi wanashindwa maisha na kuotea nyanda za majani mabichi
ughaibuni....
Wanawake ndiyo walezi wa watoto na kutokana na
mapenzi haya ya uzazi hufanya kila mbinu kutafuta namna. Kazi si nyingi
na zile chache zinazopatikana zataka elimu...Kwa wasiosoma kwenda
ughaibuni kufanya umalaya huonekana suluhisho.”
Suluhisho kweli?
Jestina George katika blogu yake anawaonya dada
wenzake wanaoangukia jehanamu hii. Jestina anakumbusha hakuna mkataba wa
kimaandishi. Ni hadaa inayopingwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Uhamiaji (IOM).
Jestina anashauri akheri uishi tu nyumbani na
umaskini kuliko kuteseka ugenini. “Wito wangu ni kwa wale ambao mna
ndugu huko na hamuelewi wanafanya nini, tafadhali fuatilieni ili
muwasaidie.”
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment