MGOMBEA urais wa Chadema ambaye pia anawakilisha Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema vyama vinavyounda umoja huo
visipochukua dola katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, havitaweza
kuchukua tena kwa miaka 50 ijayo.
Akizungumza Makao Makuu ya Chama Cha Wananchi (CUF) Buhuruni jijini Dar
es Salaam jana mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza kumpokea
alipofika katika ofisi hizo kwa mara ya kwanza, Lowassa alisema ni
lazima Ukawa wahakikishe wanashinda uchaguzi mwaka huu.
Lowassa alisema ni lazima umoja huo uhakikishe kuwa wanafanikiwa
kuingia Ikulu katika uchaguzi huu kwa sababu wakifanya kosa, hawataweza
kufanikiwa hadi baada ya miaka 50.
Kauli hiyo ya Lowassa ilikuwa ni ya kuunga mkono kauli iliyotolewa na
mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji, aliyedai kwamba balaa kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kama watashinda uchaguzi huo, litakuwa la kihistoria.
"Nimetumwa na uongozi kuja kuungana na Lowassa hadi kuhakikisha
tunaingia Ikulu. Naamini tutafika. Tusipofika mwaka huu tutasubiri miaka
50 ijayo maana hilo balaa lake kwa hawa jamaa litakawa halipimiki,"
alisema Duni, kauli ambayo Lowassa aliiunga mkono.
Lowassa aliwasifu viongozi wa Ukawa akisema ni imara na hodari kwani
pamoja na misukosuko waliyopitia, lakini wameshinda na bado wapo pamoja
wakisubiri ushindi utakaopatikana mapema asubuhi ya Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema viongozi hao wa Ukawa hawahongeki bila kufafanua ni nani
aliyejaribu kuwahonga, na kuongeza kwamba wakiendelea namna hiyo Ikulu
ni yao mwaka huu.
Alisema Ukawa watakwenda Ikulu kupitia masanduku ya kra na si kwa
maandamano akiwataka wananchi na wanaUkawa kutunza shahada za kupigia
kura.
Akizungumzia safari yake ya leo kwenda kuchukua fomu katika ofisi za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Lowassa aliwataka wanachama na wapenzi
wake kujitokeza kwa wingi akiwasihi kuwa na busara ili waondokane na
sifa ya kuitwa wakorofi.
"Wanasema tuna fujo. Sasa kesho (leo) tujitokeze kwa wingi kwenda
kuchukua fomu, lakini tuwe waungwana tusitukane wala kugombana na mtu
ili tusiwape kisingizio. Muwe na nidhamu wasipate hoja ili tuwashinde
mapema asubuhi," alisema Lowassa ambaye katika mkutano wa kutambulishwa
Ukawa, alitahadharishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa:
“Ujiandaa, maana huku kuna mabomu (ya machozi). Lakini huenda wewe
(polisi) watakuheshimu kidogo.”
Lowassa alipotaka kuwapa pole wanaCUF kutokana na kujiuzulu kwa
aliyekuwa Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, wanachama walimtaka
kuachana na suala hilo kwani wameshalisahau na hawajadhurika kwa
chochote.
Kwa upande wa mgombea mwenza wa Ukawa, Duni, alisema hawakuja kwenye
vyama kutafuta vyeo ndiyo maana aliamua kuachia nafasi ya Uwaziri na
Makamu Mwenyekiti wa CUF ili kuunganisha nguvu na Lowassa na hatimaye
kuingia Ikulu.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, alisema zimetumika nguvu nyingi za fedha
kuhakikisha Ukawa wanasambaratika lakini kwa kuwa ulikuwa mpango wa
Mungu, bado wapo pamoja na imara.
"Tumeweza kufika hapa tulipo na safari yetu imebaki kidogo tufike
tunapotaka kwa kuwa malengo yetu yanafanana na tumepata baraka kutoka
kwa Mungu ila akitokea kiongozi kati yetu akaona malengo yetu hayafai
kuliko fursa binafsi, huyo hatufai, bora aende," alisema Mbowe katika
kauli iliyoonekana kama ni kijembe kwa Profesa Lipumba na Dk. Slaa
walioondoka Ukawa.
Alisema mgombea wao wiki chache zilizopita alikuwa CCM na mgombea
mwenza alikuwa CUF lakini wamewapa nafasi kutokana na kuwa sio walafi wa
madaraka na wao ni familia moja.
Joto la uchaguzi Arusha, Mwanza nyuzi 100
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha,
Onesmo Ole Nangole, akijiuzulu wadhifa wake huo, kada mwingine wa chama
hicho, Dk. Raphael Chegeni, ametangaza kuvunja urafiki wa kisiasa na
mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Taarifa za kujiuzulu kwa Ole Nagole zimethibitishwa jana baada ya
kuwepo uvumi kwa muda mrefu kuwa alikuwa na mpango wa kufanya hivyo na
kumfuata Lowassa Chadema.
Sambamba na Ole Nangole, makada wengine walioachia uongozi ndani ya CCM
mkoani Arusha jana ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)
Mkoa, Robinson Meitinyiku na Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa, Isack
Kadogoo.
Raia Tanzania linafahamu kwamba mipango ya viongozi hao kuondoka CCM
ilianza mara baada ya vikao vya juu vya chama kulikata jina la Lowassa
mjini Dodoma katika harakati zake za kuwania urais kupitia chama hicho.
Wadau mbalimbali wa siasa za Arusha waliliambia gazeti hili jana kuwa
viongozi hao wamejiuzulu ili kwenda kuongeza nguvu ya kampeni za urais
za Lowassa ndani ya Chadema.
"Hawa waliokuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za Lowassa ndani ya CCM
na alipokatwa kugombea urais, walifedheheka sana," alisema mmoja wa watu
wa karibuna Ole Nangole.
Vikao vya mkakati wa kuhama CCM vilikuwa vikifanyika kwa siri katika
Hoteli ya Milestone jijini Arusha na jana jioni ilidaiwa kuwa walikuwa
safarini kwenda Dar es Salaam kumsindikiza Lowassa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu za kugombea urais.
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, Ferous Bano, alithibitisha
kujiuzulu kwa viongozi hao huku akisistiza kuwa ndani ya CCM kuna
viongozi mahiri zaidi ya hao waliojiuzulu na kwamba kuondoka kwao hakuna
madhara.
“Hawa (waliojiuzulu) ni kama tikiti maji. Yaani ni tunda kubwa
ukilitazama lakini ndani ni maji tu, hakuna lolote. CCM kwa sasa
haihitaji viongozi matikiti maji na itaendelea kubaki imara siku zote,"
alisema Bano.
Alisema hajasikitishwa na kuhama kwao kwani wamedhihirisha udhaifu wao katika uongozi.
Bano alisema mlango upo wazi kwa kiongozi yeyote anayetaka kuondoka CCM
huku kukiwa na taarifa kwamba yupo kiongozi mwingine atakayeondoka wiki
hii.
Chegeni amtosa Lowassa
Wakati hali ikiwa hivyo jijini Arusha, mkoani Mwanza, Mjumbe wa
Halmashuri Kuu ya CCM Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, ambaye ndiye
alikuwa kiongozi wa kambi ya Lowassa Kanda ya Ziwa, Dk. Raphael Chegeni,
ametangaza kuvunja urafiki wao huo wa kisiasa.
Akizungumza jijini Mwanza jana, Dk. Chegeni, ambaye alimshinda Mbunge
wa Busega anayemaliza muda wake, Dk. Titus Kamani kwenye kura za maoni,
alisema urafiki huo umevunjika baada ya Lowassa kuhamia Chadema na
kwamba sasa ameelekeza nguvu kubwa kushirikiana na wanaCCM wengine
kumnadi mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dk. John Magufuli.
“Siwezi kuwa na rafiki wa kisiasa nje ya CCM, rafiki yangu mzuri ni
ambaye yuko ndani ya CCM kwa hiyo Lowassa si rafiki yangu tena," alisema
Dk. Chegeni na kuongeza:
"Tulikuwa na kambi 38 za wawania urais, lakini mchakato ulikamilika
baada ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kumchagua Dk. Magufuli kuwa mgombea
wetu wa urais, huyo ndiye tingatinga la Chama Cha Mapinduzi.
"Nilimtetea Lowassa kwa sababu nilikuwa naamini atakuwa Rais, lakini
tukamchagua Dk. Magufuli, hivyo tulivunja kambi zote Dodoma na kubaki na
moja, ya Dk. Magufuli. Kwa sasa jukumu letu kubwa wanaCCM ni kumuunga
mkono akivushe chama chetu na kufufua matumaini ya Watanzania."
Akizungumzia kura za maoni Busega, Dk. Chegeni alisema mshindani wake
wa karibu, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Kamani, hana
sababu ya kulalamikia matokeo kwani katika uchaguzi suala la kushinda na
kushindwa ni la kawaida na kwamba yeye amewasamehe wote waliojaribu
kuvuruga uchaguzi huo.
Chanzo: Raia Tanzania
0 comments:
Post a Comment