OHOOO! Kimenuka tena. Mwimbaji wa nyimbo za Injili,
Flora Mbasha amesema mwanaye mdogo (jina linahifadhiwa) hahusiani hata
kidogo na aliyekuwa mumewe, Emmanuel Mbasha huku akidai kuwa anamtambua
mwanaume huyo kama mzazi mwenzake kwa mtoto mmoja tu (Liz), Risasi
Jumatano linakupa zaidi.
Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha na aliyekuwa mumewe, Emmanuel Mbasha.
Akizungumza na waandishi wetu kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki,
Flora alisema amechoshwa na manenomaneno yanayosemwa juu yake na
Emmanuel na kwamba kama mumewe huyo ameamua kumwaga ugali, yeye yupo
tayari kumwaga mboga.
Mwimbaji huyo alisema kwamba kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa
anampenda mumewe na kwamba yupo tayari kuishi naye haikutoka moyoni,
isipokuwa alifanya hivyo kwa huruma tu, kwa sababu mwanaume huyo ni mtu
katili, mwenye roho mbaya na asiyemuogopa Mungu.
“Mtu mwenyewe alimtelekeza mtoto (Liz) kwa zaidi ya mwaka mmoja, ni
mtu mbaya sana, sina mapenzi na Mbasha hata kidogo, ni afadhali niolewe
na chizi anayeokota makopo kuliko kurudiana na mtu katili na mnyama kama
huyo, namheshimu kama mzazi mwenzangu kwa Liz,” alisema.
“Huyo mwanaume hafai kabisa, ni katili, namfananisha na shetani,
anajifanya mwema kwa watu wakati hajawahi kuiomba msamaha familia,
sikubaliani kabisa na hukumu ya mahakama, ukweli anaujua kwamba alibaka
na hata mkimtaka huyo binti mumhoji nitamleta, isitoshe sasa hivi hata
mtoto wake hamjali, hajui anasoma vipi, hajawahi kulipa hata shilingi ya
ada, mimi mwenyewe ndo nahangaika kumlea mwanangu Liz ambaye anasoma
kidato cha kwanza.
“Hastahili kabisa kuitwa baba sababu mzazi mwenye akili hawezi
kutelekeza familia hata kama tumegombana, nimemwachia nyumba niliyojenga
kwa pesa yangu na pesa zote aliweka kwenye akaunti yake na zote
nilimwachia lakini kashindwa kuihudumia familia.”
Flora anajulikana kuwa na watoto wawili, mdogo akiwa ni yule
aliyezaliwa wakati wanandoa hao wakiwa katika mzozo uliosababisha
watengane hadi hivi sasa. Alipoulizwa kwa nini anadai aliyekuwa mumewe
kumtelekeza mtoto mmoja tu, badala ya wawili, alifunguka.
“Huyu mwanangu mdogo hausiki naye kabisa, tena asiwe anamtaja kabisa
kwa sababu hamhusu, hajui hata matumizi yake yakoje, mengine kaka achana
nayo tu,” alisema Flora.
Mwimbaji huyo mwenye kipaji alipoulizwa sababu za kufuta kesi ya
kudai talaka, aliyoifungua hivi karibuni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, wakati anadai hamtaki na hawezi kurudiana naye, alisema
alifanya hivyo baada ya kushinikizwa na mtu ambaye hata hivyo, alikataa
kumtaja.
Flora alisema familia yake haijaridhishwa kabisa na suala la kesi ya
ubakaji iliyokuwa ikimkabili mumewe kumalizika kwa kuachiwa huru na
kwamba wanajipanga kwa ajili ya kukata rufaa.“Hiyo kesi imeisha kisiasa,
Mbasha aliwahi kukiri kuwa ni kweli alifanya kitendo hicho, iweje leo
aonekane hana hatia? Tutakwenda kukata rufaa ili haki itendeke.”
Baada ya kuzungumza na Flora, mwandishi wetu alimtafuta Mbasha kwa
lengo la kumuuliza kuhusu madai ya mtoto yule mdogo kutohusika naye kama
alivyosema mkewe, naye bila ‘kutafuna maneno’, alisema hata yeye
hamtambui huyo mtoto mdogo, ila anaomba arudishiwe mtoto wake mkubwa,
Liz na maisha mengine yaendelee.
“Hata mimi simtambui huyo mwingine, ninachoomba anirudishie tu mtoto
wangu mkubwa Liz, huyo mwingine sihusiki naye kabisa kama alivyosema,
yeye (Flora) ndiye anajua mhusika wa huyo mtoto, lakini si mimi na wala
hajakosea kusema hivyo, nililitambua hilo tangu zamani, anipe tu
mwanangu wa kwanza,” alisema Mbasha.
chanzo: global publishers
0 comments:
Post a Comment