LATEST POSTS

Tuesday, February 23, 2016

Babu Loliondo ajiandaa kwa mafuriko mapya

  • Aanza kujenga nyumba za wageni eneo la eka 70
  Asema muujiza wa sasa ni zaidi ya tiba ya `kikombe`

Baada ya kimya cha muda mrefu, Mchungaji mstaafu, Ambilikile Masapila (82) maarufu kama ‘Babu wa Loliondo’, ameibuka upya na kuwataka Watanzania wajiandae kwa ‘mafuriko’ ya watu watakaomiminika nyumbani kwake kutoka katika mataifa mbalimbali duniani, kufuata huduma itokanayo na muujiza mkubwa zaidi kulinganisha na ule wa tiba ya kikombe uliomtokea mwaka 2009.
Akizungumza juzi katika mahojiano maalum na Nipashe nyumbani kwake Samunge, Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Masapila alisema kwa mara nyingine, Watanzania wajiandae kupokea habari njema kuhusiana na muujiza mkubwa wenye kuleta suluhisho la matatizo mengi ya binadamu, na hivyo kulitangaza jina la nchi yao (Tanzania) kote ulimwenguni.

'Babu' alisema ujiuo wa ‘mafuriko’ hayo ya watu utaanza hivi karibuni na ameshaanza maandalizi kabambe ya kupokea ugeni huo utakaokuwa wa kihistoria.

Hata hivyo, Babu Masapila hakutaja ni lini hasa ataanza kutoa huduma hiyo itokanayo na muujiza mpya, bali alisisitiza kuwa “ni hivi karibuni”, hasa atakapokuwa amekamilisha maandalizi ya mahala pa kupokea wageni.

“Nilipata maono ya jambo hili mwishoni mwa mwaka uliopita (2015). Ni ndoto inayohusiana na habari njema kwa binadamu, ni ndoto iliyonilazimu kuanza maandalizi ya kupokea watu wengi zaidi na ndiyo maana nimeanza maandalizi,” alisema Babu Masapila, anayesisitiza kuwa yeye hupata nafasi ya kuzungumza na Mungu (wake) mara kwa mara kupitia ndoto.

Anasema kila anachokifanya hutokana na maagizo anayoyapata kupitia sauti kutoka kwa Mungu.

Hadi kufikia mwaka 2011, Babu Masapila alikuwa gumzo nchini na nje ya mipaka kutokana na huduma yake ya tiba ya kikombe iliyovutia maelfu ya watu.

Dawa hiyo aliyodai inatibu maradhi mengi yakiwamo ya kisukari, aliitoa kupitia kikombe na kuiuza kwa Sh. 500 tu.

Iliwateka watu wa kila namna wakiwamo wanasiasa, viongozi wa kidini, wasanii maarufu, wafanyabiashara na wakuu wa vikosi mbalimbali vya majeshi.

Inakumbukwa kuwa miongoni mwa vigogo waliowahi kufika kwa Babu na kupata ‘kikombe’ ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Rais John Magufuli,  ambaye baada ya kunywa dawa aliwaambia watu waliojazana eneo hilo kwa maelfu kuwa serikali itatumia Sh. bilioni 1.05 kutengeneza barabara inayoingia kijijini hapo ili kurahisishia usafiri kwa watu wanaokwenda kwa Babu Masapila.

Wengine waliowahi kufika ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Askofu Thomas Laizer ambaye sasa ni marehemu.

Ingawa watu waliomiminika kwake mwaka 2011 kwa ajili ya kupata tiba ya ‘kikombe’ walitengeneza msururu mrefu wa magari uliofikia kilometa 15, Babu Masapila alisema watu watakaokwenda kwake sasa kutokana na muujiza mpya watakuwa wengi maradufu na ndiyo maana ameanza kujenga nyumba za kutosha ndani ya eneo lenye ukubwa wa eka 70 ili kuwapokea.

“Kupitia ndoto hiyo niliagizwa kutafuta eneo kubwa na kujenga nyumba za kutosha kwa ajili ya kupokea wageni kabla ya kuanza kutoa huduma," alisema Babu Mwasapila katika mahojiano.

"Nashukuru uongozi wa kijiji (cha Samunge) umenielewa na kuniunga mkono kwa kunipatia eneo nililoelekezwa kwa kazi hiyo (kupitia ndoto).”

Akieleza zaidi, Babu Masapila alisema sauti kupitia ndoto yake ilimuelekeza kujenga nyumba za kupokea wageni katika eneo la jirani na Mlima wa Makao na hivyo, anaushukuru uongozi wa serikali ya kijiji kwa kumpatia eka 70 hizo kandoni mwa mlima huo na tayari ameanza ujenzi wa nyumba hizo.
“Namshukuru sana Mungu. Ana mpango maalumu na Tanzania kupitia Samunge. Naona Tanzania inakwenda kuwa maarufu barani Afrika kupitia Samunge.

"Kutafanyika miujiza mingi na dunia nzima itaijua Tanzania, tena kuliko ule muujiza wa kikombe.“

Babu Mwasapila ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Akieleza zaidi maandalizi hayo ya kupokea ugeni mkubwa zaidi, Babu Masapila alisema tayari kuna nyumba sita ameshazijenga na ziko katika hatua ya mwisho ya kukamilika.

Alisema kazi hizo zinarahisishwa na malori mawili aina ya Fuso aliyoyanunua kitambo kwa shughuli za kubeba mchanga na vifaa vya ujenzi, na pia kubebea kuni za kuchemshia dawa zake.

Aidha, gari lake la kutembelea aina ya Toyota Land Cruiser hutumika pia kwa shughuli za kubebea dawa mbalimbali za uponyaji. 

Babu Masapila anasema hivi sasa amewaajiri watu 13 ambao huwalipa mishahara kuanzia Sh.100,000 kwa mwezi ili kusaidia maandalizi hayo. 

Masapila alisema tangu alipopata maono kuhusu maandalizi ya kupokea ugeni wa watu wengi zaidi, kila anapolala huona makundi ya watu waliosongamana pembeni mwa Mlima Makao na ndiyo chanzo cha kuliomba eneo hilo.

Diwani wa Kata ya Samunge, Kajulus Steven, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, anakiri kijiji kumpatia Babu Masapila eneo la eka 70, kandoni mwa Mlima Makao ili afanye maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wageni.

Alisema walimpa eneo hilo baada ya Babu Masapila kuwaeleza kuwa kuna muujiza mwingine hivi karibuni.
“Tulishajifunza kutokana na kile kilichotokea mwaka ule… alituambia anaona watu wakifurika Samunge lakini sisi hatukujali, tukapuuza maono yake.

Mwishowe watu wakafurika kweli, tukahangaika sana,” alisema Steven na kuongeza:

“Kwa sababu hiyo, safari hii tumemsikiliza na kumpatia eneo alilodai kuoteshwa kuwa ndilo linalofaa kwa huduma.
"Viongozi wa eneo hili tulikaa na kuingia naye makubaliano kuwa akimaliza kutoa huduma zake hizo tutalirejesha.”

Steven alisema wanamchukulia Babu Masapila kama ‘nabii’ kwa sababu mambo mengi aliyowahi kutabiri kuwa yatatokea, yametokea kweli, ikiwamo kupata umeme ambao hivi sasa umewafikia kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na kufikishwa kwa huduma za simu za mkononi baada ya kufungwa kwa minara ya kampuni mbili.

HIVI SASA HALI IKOJE?
Akizungumzia hali ya utoaji huduma za uponyaji hivi sasa kulinganisha na vile ilivyokuwa wakati wa ‘mafuriko’ yaliyotokana na tiba ya kikombe, Babu Masapila alisema ipo tofauti kubwa.

Alisema wakati huo, watu aliokuwa akiwapatia kikombe walikuwa wakifika hadi 18,000 kwa siku lakini hivi sasa idadi hiyo imepungua hadi kuwa chini ya watu 20 kwa siku.

“Hivi sasa nawahudumia (watu) 10 hadi 20 na kwa sababu kila mmoja hulipia Sh. 500, mwanzoni fedha zilizopatikana zilifikia hadi Sh. milioni tisa kwa siku… lakini hivi sasa kiasi kinachopatikana ni kati ya Sh. 5,000 na 10,000,” alisema.

Akieleza sababu za kupungua huko kwa wateja, Babu Masapila alisema hashangazwei kwa sababu anaamini kuwa huo ni mpango maalum wa Mungu.

“Sishangazwi. Mungu mwenyewe amependa kusitisha umaarufu wa huduma hii (tiba ya kikombe) ili nipate muda wa kufanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea watu wengi zaidi watakaofika hapa (Samunge) kuliko wale wa awali,” alisema Babu Masapila.

FAMILIA, HISTORIA
Babu Masapila aliiambia Nipashe kuwa yeye ni baba wa watoto wanne, kati yao watatu ni wa kiume na kwamba, hivi sasa familia yake bado iko Babati mkoani Manyara.

Alisema kabla ya kufika Samunge, alikuwa wilayani Rungwe, mkoani Mbeya. Mwaka 1952 aliondoka (Mbeya) na kwenda Korogwe mkoani Tanga kabla ya kuhamia Babati na kisha kutua Samunge alikokuwa akifanya kazi ya uchungaji wa KKKT.

Alisema baada ya Mungu kumpa nguvu ya uponyaji kupitia kikombe, sasa bado anaendelea kutoa huduma hiyo kwa watu mbalimbali, wengi wanaoendelea kufika kwake wakitokea Dodoma na nchi za Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Eritrea.

HALI KIMAISHA
Baada ya kufika nyumbani kwa Babu Masapila na kuonyeshwa mahala anapoishi sasa na pale alipokuwa akiishia awali kabla ya mwaka 2011, mwandishi alibaini kuwa Babu Mwasapila ameimarika zaidi kiuchumi.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa awali alikuwa akiishi katika nyumba ndogo ya udongo lakini sasa anaishi kwenye nyumba kubwa na ya kisasa huku pia akitembelea Land Cruiser na kumiliki malori mawili aina ya Fuso, achilia mbali muonekano wake unaoshiria kuwa ni mtu mwenye afya tele.

Aidha, Babu ana mradi wake wa ujenzi wa nyumba sita za kisasa na miundombinu mingine kwa maandalizi ya kupokea maelfu ya wageni kwenye eneo la eka 70.

Mbali na malori yake kumsaidia katika shughuli za maandalizi ya ujenzi wa nyumba za kupokea wageni, pia vyombo hivyo huvikodisha kwa shughuli za ujenzi na hivyo kumuongezea kipato kinachotumika kuboresha huduma zake.
  
UJIO WA VIONGOZI, WANASIASA
Kuhusiana na namna alivyojisikia baada ya kupata ugeni wa viongozi mbalimbali mashuhuri na watu kutoka nje ya nchi kufuata tiba yake ya kikombe, Babu Masapila alisema hayuko tayari kuzungumzia hilo kwani siyo vizuri kujadili majina ya wale waliowahi kupata huduma yake. 

Hata hivyo, alisema anafurahi kuona kuwa wapo wakubwa wengi wanakubali tiba ya kikombe chake na kuiamini kwani ndiyo msingi wa kupona kwa kila anayepata huduma hiyo.

MTI WA DAWA
Akiuzungumzia mti wa dawa ya kikombe, Babu Masapila alisema siyo mpya na wengi wanaufahamu kwa majina taofauti.

“Mti wa dawa ninaotoa unajulikana kwa majina tofauti kulingana na makabila husika. Wairaqw wanauita Titiwi, Wakurya wanaita Mkarakara na Wamasai wanauita Ngamriaki," alisema.

"Siyo kwamba mimi nimeubuni na sikujua kama unatibu, hapana. Mungu aliweka neno na akanionyesha mimi… mtu akinywa kikombe kimoja tu anapaswa kupona.”

Hata hivyo, aliongeza kuwa kama mtu hajapona vizuri, hazuiwi kurudia kunywa kikombe, lakini kwa sharti kwamba siyo kwa siku hiyo bali siku nyingine, hasa baada ya kupita siku saba zinazopaswa kuwa za uponyaji.

Alisema mhusika anapaswa kwenda kupimwa kama maradhi yanayomsumbua yameisha ama la ndani ya kipindi cha miezi mitatu hadi minne.

Alisema wapo baadhi ya watu humpuuza na kumdharau, lakini hilo halimsumbui ila anawasamehe na kumuachia Mungu kwani anajua kuwa wengi wa wanaombeza ni waganga wa jadi wanaohofia kupoteza wateja, na wakuu wa makanisa ya baadhi ya madhehebu ambao huhofia kupoteza waumini wao wenye nia ya kuombewa ili wapate nafuu ya matatizo mbalimbali ya kiafya.

TUHUMA ZA KUSABABISHA VIFO
Babu Masapila alisema anatambua kuwa baadhi ya watu wanaompinga huvumisha kuwa dawa ya ‘kikombe’ chake ilisababisha vifo.

Akielezea kuhusu hilo, alisema hakuna ukweli bali wapo baadhi ya wagonjwa walifariki baada ya ndugu zao kuwatorosha kutoka katika hospitali mbalimbali walikokuwa wamelazwa, na kuzidiwa wakati wakiwa kwenye foleni ya kupata kikombe cha dawa.

“Wengi kati ya wale waliobahatika kupata kikombe walipata nafuu na afya zao kuimarika,” alisema.

Hata hivyo, haitashangaza kusikia kuwa wapo pia watu waliokunywa dawa ya kikombe chake na bado wakafariki dunia, alisema Babu Masapila, kwani yeye hana dawa ya kuzuia kifo.

Alisema hata kwenye hospitali zote duniani wapo watu hupona na wengine hufariki kwa sababu Mungu ndiye huamua hatma ya maisha ya kila binadamu.

Alisema wakati watu walipokuwa wakifurika kwake kufuata tiba ya ‘kikombe’, kuna wataalamu waliojitambulisha kuwa wanatoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali walifika na kuchukua sampuli ya dawa na kwenda kuifanyia utafiti na hakukuwa na majibu yaliyodai dawa hiyo ina madhara.

Babu Mwasapila alisema kuwa wataalamu hao walifika tena na kuchukua mizizi ya mti anaoutumia kwa maelezo kuwa wanakwenda kuchunguza ili kujua ni baada ya muda gani dawa hiyo huua virusi na vimelea vingine vya magonjwa mbalimbali baada ya mtu kuinywa.

“Cha kushangaza, watu hao hawajarudi tena kwangu… kwa hiyo sijui kinachoendelea.”

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Samunge, Simon Dudui, watu 52 walifariki dunia wakati wakiwa kwenye foleni ndefu kusubiri huduma ya ‘kikombe cha babu’ mwaka 2011.

MATUNDA YA ‘KIKOMBE‘ SAMUNGE
Diwani Steven wa Kata ya Samunge, alisema huduma ya kikombe cha Babu Masapila ilileta maendeleo makubwa na ya ghafla kwao, hasa kuhusiana na barabara, upatikanaji wa maji safi na pia kuinuka kiuchumi kwa baadhi ya wakazi wake.

Alisema kabla ya kikombe cha babu, Samunge hakukuwa na mahala pa kulala wageni na yeyote anayehitaji huduma hiyo alilazimika kwenda Loliondo ambako ni mbali, lakini sasa hali ni tofauti kwani tatizo hilo halipo tena.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Samunge, Jonath Kilobei, alisema ‘kikombe cha babu’ hawatakisahau kwani kimewainua kimaisha kutokana na biashara walizokuwa wakifanya wakati watu walipofurika na kwamba sasa, wanasubiri kwa hamu ujio wa mkubwa zaidi wa wageni kama Babu Masapila alivyowaahidi.

Afisa Mtendaji Dudui, alisema mbali na maandalizi binafsi ya Babu Masapila, wao pia wameanza maandalizi ya kupokea maelfu ya watu kwa kuimarisha huduma za zahanati yao ya Samunge kwa kuipanua na pia kuongeza madaktari wawili.

“Pia kijiji kimetenga eneo la ujenzi wa vyoo na stendi kwa ajili ya kuingiza magari mengi kwa wakati mmoja,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa tayari kijiji cha Samunge kimeanzisha vikundi vya ulinzi na usalama na pia kununua matanki kadhaa ya maji yenye ujazo wa lita 1,000 kila moja ili yasambazwe kwenye maeneo yaliyo karibu na eneo la Babu.

“Hatutaki tena aibu ya wakati ule wa ujiuo wa watu wengi. Tulikuwa tunafanya kazi kwa zimamoto baada ya kupuuza maelezo ya Babu. Hivi sasa tupo naye karibu na tumejipanga mapema kupokea watu wengi zaidi,” alisema Afisa Mtendaji huyo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa Kijiji cha Samunge, Aden Sinodia Gibaseya, alisema yeye ni miongoni mwa watu walionufaika kibiashara wakati wa muujiza wa ‘kikombe cha babu’ kwa kuuza maji na vyakula.

Mfanyabiashara mwingine aitwaye Sam Alen Ndugai, alisema naye ni miongoni mwa watu walionufaika sana kwa kuuza vyakula na maji na alikuwa akiingiza hadi Sh. milioni 28 kwa siku.

Hata hivyo, anasema alipata pigo kubwa baadaye wakati shehena ya maji aliyokuwa akiyauza Sh. 4,000 kubaki mikononi mwake kufuatia umati uliokuwa ukifika Samunge kila uchao kupotea ghafla.

“Babu alisisitiza kwamba tusiuze bidhaa zetu kwa bei kubwa. Wengi hatukumsikiliza… tukawa tukiuza chupa moja ya maji kwa Sh. 4,000," alisema Ndugai. "Nilipata fedha nyingi, lakini nyingi zikapotea pia baada ya kununua bidhaa kibao na kubaki nazo ndani wakati kasi ya watu kufuata kikombe ikikatika ghafla.

"Safari hii kama wageni wakija tena kwa wingi nitakuwa makini na kuzingatia ushauri wa Babu.”

Kina mama waliojitambulisha kwa majina ya Esuvati Loishiye na Anna Laizer, walisema Babu amesaidia kubadilisha hali ya Samunge kupitia tiba ya kikombe kwa sababu tangu wakati huo, hivi sasa wameamka na kuchangamkia biashara ya kupika na kuuza chakula.
Chanzo: IPP Media

Friday, February 19, 2016

WANAFUNZI WALIOONGOZA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE 2015 KITAIFA




Huyu ndiye Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza Kitaifa katika Mtihani wa Kidato cha Nne kutoka shule ya Canossa Girls.Anaitwa Butogwa Charles Shija(17), akiwa mwenye furaha, nyumbani kwa wazazi wake Kipunguni Jijini la Dar es Salaam jana.Anasema  kilichomsaidia kufanya vizuri ni kufanya marudio,kumwomba mungu na kujiwekea lengo la kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.Mama yake mzazi anaitwa Angela Shija ambaye anasema binti yake tangu akiwa kidato cha kwanza aliahidi kufanya vizuri katika mtihani na amekuwa na juhudi za kujisomea kila wakati.Jina Shija ni maarufu sana kwa kabila la Kisukuma



Huyu ni Mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne Feza Girls 2015 , Mtanzania mwenye asili ya China, Congcong Wang,ameshika Nafasi ya pili Kitaifa ,amepata alama  'B' somo la Kiswahili .Alijiunga na shule hiyo mwaka 2006 akitokea China na Kulazimika kujifunza lugha tatu ambazo ni Kiswahili,Kiingereza na Kituruki ambazo hutumika katika shule hiyo ili aweze kuwasiliana na wenzake vizuri pamoja na walimu wake.
 
 Anasema: Walinisaidia wakijua baadhi ya vitu sitaelewa,cha muhimu ni kwamba hakuna njia ya mkato zaidi ya kusoma

Wednesday, February 17, 2016

Kitunguu Swaumu, Mafuta ya Mzaituni kwa kutibu sikio


kitunguu swaumu 
Wiki hii utaelekezwa namna unavyoweza kutibu sikio kwa kutengeneza dawa nyumbani kwako ambayo ni mafuta ya mzaituni na kitunguu swaumu.
Vitu vinavyohitajika
Punje moja ya kitunguu swaumu iliyosagwa na vijiko 2 vya mafuta ya mzaituni
Oleacanthal-the-key-benfit-of-olive-oil 
Jinsi ya kutengeneza dawa
Njia ya kwanza ni ya kupasha moto mafuta ya mzaituni kisha kuchanganya na kitunguu kilichosagwa. Mchanganyiko huu unaachwa upoe, kisha unadondoshwa kwenye sikio. Hii hutibu na kutuliza maumivu haraka kutokana na ujoto wa dawa hiyo.
Njia ya pili ni kuchukua kitunguu swaumu, kukisaga kisha kuchanganya na mafuta ya mzaituni, halafu mchanganyiko unaachwa kwa saa mbili hadi tatu, kabla ya kutumika. Baada ya kutengenezwa kwa dawa hii, mtumiaji atatumia kwa kudondoshea matone mawili sikioni wakati wa asubuhi na atafanya hivyo tena jioni. Ni dawa isiyo na madhara kwa mtumiaji.
Hatua hii ya pili si rahisi sana kukupa ahueni kama hiyo ya kwanza.

Source: Global publishers

Saturday, February 13, 2016

Mwanamke Aliyepambana na Kunyang’anya Bunduki Jambazi Azawadiwa Laki 5

RISASI MAJAMBAZI MWANAMKE (4)Sophia Manguye akisaini mara baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo.

Mwanamke aliyepambana na jambazi na kufanikiwa kumnyang’anya bunduki aina ya SMG, Sophia Manguye (46), amepewa zawadi ya Sh 500,000 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Gemini Mushy.
Mwanamke huyo ambaye aliomba Serikali kumpa silaha ili kujilinda, alisema kuwa hajaridhika na zawadi hiyo kwa kuwa kama asingemmudu jambazi huyo watu wengi wangepoteza maisha.
Hata hivyo, Mushy alimwomba Manguye kupokea kiasi hicho japokuwa ni kidogo kwa kuwa ni zawadi kutoka ofisi yake.

RISASI MAJAMBAZI MWANAMKE (5)Sophia Manguye akihojiwa na wanahabari.
Tukio hilo lilitokea Februari 9, saa 2.42 usiku, baada ya watu watatu kufika dukani kwake, mmoja wao akiwa na bunduki kisha kumwamuru atoe fedha alizokuwa nazo.
Manguye alisema alichukua Sh80,000 alizokuwa nazo na kumkabidhi jambazi huyo, lakini hakuridhika na kumlazimisha aongeze kiasi kingine.
“Nilipandwa hasira nikanyanyuka wakati jambazi anainama kuangalia kwenye kiboksi cha fedha, nikamkamata kifuani na kung’ang’ania mkanda wa bunduki, akaanza kunivuta kwenda nje, nami nikamvutia ndani, lakini alifanikiwa kunitoa nje akaniangusha chini, lakini sikuachia mkanda wa bunduki,” alisema Manguye na kuongeza: RISASI MAJAMBAZI MWANAMKE (1)“Aliposikia wananchi wameanza kupiga yowe akaniachia na kutoa mkanda wa silaha begani, akakimbia na kuniachia bunduki. Wakati huo huo jambazi mwingine alikuwa amekamatwa kwenye duka la Zaituni Magasi, wananchi walipofika wakaanza kumshambulia, wakati huo taarifa ilikuwa tayari imetolewa Kituo cha Polisi Sirari, wakafika kumchukua,” alisema.

RISASI MAJAMBAZI MWANAMKE (2)Hii ni mara ya pili kwa Manguya kuvamiwa na majambazi wenye silaha, ambapo mwaka 2014 alivamiwa dukani kwake na majambazi waliokuwa na bunduki, lakini alifanikiwa kumpiga kwa kigoda aliyekuwa na bunduki na alianguka chini.
Magasi alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa amevamiwa na majambazi waliokuwa na bunduki, mapanga na nondo.
“Wakati anatoka mvunguni mdogo wangu alimkamata kwa nyuma na kummudu huku akipiga kelele, watu wakafika wakaanza kumpiga hadi akazimia, polisi walipofika wakamwokoa kwani kidogo wamuue,”alisema.

Source:Global Publishers

Friday, February 12, 2016

Siku 100 safi za Rais Magufuli

LEO ni siku ya 100 tangu Rais John Magufuli alipoingia Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, na tangu alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, ameishi katika maneno yake kwa kutenda kile anachokisema.
Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la dawa za kulevya, akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo akaahidi kushughulikia mtandao huo na wakubwa wanaohusika. Kwa upande wa rushwa, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ufisadi na rushwa na katika kutekeleza hilo, alisema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia wezi wakubwa yaani mafisadi. Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi wazembe ili Serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu wakati hawafanyi kazi yoyote.
Katika kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo hazina umuhimu katika Serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi. Aliahidi pia kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Rais Magufuli pia alisema Serikali yake itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato, ukizingatia kuwa kodi ni kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.
Aliahidi kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai vimegeuzwa mazizi ya mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya kuviendeleza. Aliahidi pia kushughulika na kero zinazolalamikiwa kutendwa na polisi, hospitali, mizani, Mahakama, maliasili na vilio vya wachimbaji. “Inabidi haya yote niyataje ili nijue tunaanzia wapi na tunakwenda wapi, nisipoyataja nitakuwa mnafiki,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 mjini Dodoma.
Tayari Rais Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania. Amebana matumizi ya serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija, matumizi yasiyo ya lazima, ameshughulikia watumishi wazembe, ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na kutoa elimu ya bure. Alivyoanza kazi Mara tu baada ya kuingia ofisini, alimuapisha Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya kuapishwa.
Kesho yake, Rais alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha ambako aliagiza maofisa wa wizara hiyo, kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hususan kwa wafanyabiashara wakubwa bila kuogopa. Akataa mchapalo wa Bunge Rais alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya sherehe ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh milioni 251, ambazo aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Jumla ya vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695. Afuta gwaride la Uhuru Rais Magufuli pia alifuta gwaride la Siku ya Uhuru, badala yake akaamuru siku hiyo iadhimishwe na wananchi wote kwa kufanya usafi maeneo yanayowazunguka ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.
Wananchi waliitikia agizo hilo kwa wingi na kufanya usafi mkubwa. Fedha Sh bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Siku ya Uhuru, ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3, kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Ujenzi wa barabara hiyo tayari umeanza. Majipu yalivyotumbuliwa Rais alianza kazi ya kutumbua majipu siku yake ya nne akiwa ofisini, alifanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako alijionea huduma zilizozorota hospitalini hapo na hivyo akalazimika kuivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na kumuondoa madarakani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Hussein Kidanto.
Mamlaka ya Mapato Baadaye Waziri MKuu Kassim Majaliwa alifanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam, ambako aligundua upotevu wa makontena 329. Hatua iliyosababisha Rais kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kumteua Dk Phillip Mpango kukaimu nafasi hiyo. Kabla ya Bade, Majaliwa alishatangaza kuwasimamisha kazi Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.
Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema. Majaliwa pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo, wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni, lakini baadaye akabadilisha uamuzi wake na kuamuru watumishi hao nao wasimamishwe kazi.
Upotevu huo wa makontena pia ulisababisha TRA kuwasimamisha kazi watumishi wake 35 na kampuni 43 za uwakala wa forodha, zilisimamishwa kwa tuhuma za kuhusika kutorosha makontena hayo. Uchukuzi, Bandari na Reli Baada ya kubainika matumizi ya Sh bilioni 13 za Kampuni ya Reli (TRL) kutumika kiholela, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Pia Rais siku hiyo aliivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), iliyokuwa chini ya Profesa Joseph Msambichaka kutokana na kubainika madudu mengi bandarini hapo. Rais pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe. Takukuru Katika kutimiza ahadi yake ya kupambana na ufisadi, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea.
Alimteua Naibu Mkurugenzi Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo. RAHCO Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito naye alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati. Licha ya kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Rais Magufuli pia aliivunja Bodi ya Rahco.
Vitambulisho vya Taifa Kutokana na malalamiko ya kusuasua kwa utoaji wa vitambulisho vya Taifa, Rais pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na kuwasimamisha kazi maofisa wengine wanne wa taasisi hiyo.
Maofisa wanne wa NIDA waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa namna Sh bilioni 180 zilivyotumiwa na mamlaka hiyo wakati wananchi waliopatiwa vitambulisho vya taifa na mamlaka hiyo ni wachache ni Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.
Mabalozi Rais pia aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili, ambao mikataba yao iliisha. Mabalozi hao ni Batilda Buriani aliyeko Tokyo nchini Japan na Dk James Msekela aliyeko Rome, Italia. Rais alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe.
Balozi huyo anarejea wizarani ambako atapangiwa kazi nyingine. Uhamiaji Madai ya kukithiri kwa rushwa katika Idara ya Uhamiaji pia kulimfanya Rais Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na Fedha, Piniel Mgonja ili kupisha uchunguzi katika idara hiyo nyeti nchini.
Elimu bure yaanza Katika siku zake 100 akiwa Ikulu, Rais Magufuli ametenga Sh bilioni 137 kwa ajili ya kugharimia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni mwakani. Elimu bure inatolewa kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne

Thursday, February 11, 2016

Fahamu Ugonjwa wa Zika na dalili zake


children-born-with-microcephaly

Homa ya Zika ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus.” Na Ugonjwa huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana/jioni. Aina hii ya kirusi ipo katika familia ya (Flavirus)  ambapo pia vipo virusi vya ugonjwa wa dengue, Homa ya Manjano (Yellow Fever).
Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, makopo nk.

Dalili zake
Dalili za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya Dengue, ambazo ni homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na vilevile kupata vipele vidogo vidogo kama harara (Skin rashes).
Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 2 hadi 7 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya Zika.
Wakati mwingine wagonjwa wanaweza kupata matatizo katika ubongo (Neurological Complications) na miguu kupooza (Gullein Barre Syndrome) na wajawazito huweza kujifungua watoto wenye ulemavu wa kichwa yaani kichwa kuwa kidogo kulingana na umri wa mtoto  kitaalam Microcephaly.
Dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria. Hivyo basi, mtu anapojisikia homa ahakikishe anapima ili kugundua kama ana vimelea vya malaria au la.

 Itaendelea

Kivuko cha MV Kigamboni chazua taharuki

mv kigamboni (2)
Abiria wakiwa wamekumbwa na taharuki baada ya kivuko cha MV Kigamboni kuacha njia leo asubuhi.

Abiria waliokuwa wakisafiri ndani ya Kivuko cha MV Kigamboni jijini Dar es Salaam  mapema leo wamekumbwa na taharuki huku wengine wakijitosa majini baada ya kivuko hicho kupoteza mwelekeo na kuacha njia majini.
Inadaiwa chanzo cha taharuki hiyo ni kuzidisha abiria pamoja na mizigo kwenye kivuko hicho.

mv kigamboni (1)Abiria wakipewa maelekezo jinsi ya kutoka kwenye kivuko hicho

Wednesday, February 10, 2016

Hatua 7 za kukabiliana na nyakati ngumu maishani


Businessman with head in hands
SHIDA ni sehemu ya maisha ya binadamu. Katika dunia hii kuna wakati maisha hujaribu kuleta kila aina ya vizingiti na kama hutasimama katika mstari imara ni rahisi kushindwa.
Kila kitu huonekana kwenda mrama, na baadhi yetu hufikia hatua ya kukata tamaa na kuamua kuyaacha mambo yaende kama yalivyo, kitu ambacho si sahihi sana maishani.
Wakati mwingine ili uweze kusimama katika misingi imara kimaisha, basi ni lazima ukutane na vizingiti, dhoruba na vikwazo ikiwa ni moja kati ya njia za kukukomaza kimaisha.
Kuna vitu vikuu viwili maishani ambavyo mtu hawezi kuepukana navyo kwa namna yoyote ile, navyo ni Furaha na Huzuni. Hivi ni vitu ambavyo kila mtu huvipitia, lakini cha kushangaza, watu wengi sana hupenda kukutana na furaha na inapokuja hali ya maumivu, basi wengi wetu hunyong’onyea na kuwa dhaifu katika utendaji wa mambo.Hapa chini kuna badhi ya mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa ili kukabiliwa na wakati mgumu.

KUBALIANA NA HALI HALISI
Pindi unapokuwa unakabiliana na wakati mgumu maishani mwako, usikimbilie kukata tamaa, hatua ya kwanza kufanya ni kukubaliana na ukweli wa hali yenyewe ilivyokupata.
Kamwe hiki si kipindi cha kulaumu, hata kama wewe ndiyo chanzo cha tatizo hilo, bado hupaswi kujilaumu kwa kile ulichokifanya. Lakini pia usilipe nafasi kubwa tatizo hilo katika akili yako, kwani kufanya hivyo ni kuzidi kulikuza. Kuwa mtulivu tafuta njia ya kulitatua.

USIMWELEZE KILA MTU
Watu wengi hukosa uvumilivu pindi wanapokuwa katika nyakati ngumu maishani na kujikuta wakigeuka waropokaji kwa kila mtu wakidhani kwa kufanya hivyo kutasaidia kutatua matatizo yao, jambo ambalo si kweli.
Pamoja na ukweli kwamba matatizo huhitaji msaada wa kimawazo kutoka kwa watu wengine lakini si kwa kila mmoja unayekutana naye au kumuona. Jaribu kuwafuata baadhi ya watu ambao unaamini kuwa wanaweza kuleta suluhu, ukimweleza kila mtu ni rahisi kupata ushauri wa kukuvunja moyo.

USIKAE BILA KUJISHUGHULISHA
Epuka sana kukaa bila kujishughulisha kiakili na kimwili kila wakati ili kuitokomeza hali ya huzuni na maumivu unayokabilian navyo kwa kipindi hiki.
Pendelea kufanya baadhi ya vitu vinavyoweza kukuletea faraja na furaha, mfano labda kujisomea baadhi ya maandiko yatakayokupa mwanga, fanya mazoezi, angalia hata mechi mbalimbali za mpira pamoja na mambo ambayo unaamini ukiyafanya utapata mwelekeo mpya kimtazamo.

EPUKA MFADHAIKO
Hupaswi kukaa peke yako muda mrefu, kwani kwa kufanya hivi unakaribisha mfadhaiko akilini mwako kutoka na ugumu wa kimaisha unaokutana nao. Changamana na makundi ya watu wenye furaha ili wakusaidie kuponya huzuni yako.

JIAMINI, TUMIA UWEZO WAKO WOTE
Ndani yako kuna uwezo mkubwa sana ambao ukiutumia kikamilifu, unaweza kutatua baadhi ya mambo bila hata ya kuhitaji msaada kwa mtu mwingine. Unapaswa kujiamini. Usiwe na mashaka na uwezo ulionao ndani yako. Tambua maisha ni safari na dereva wake ni wewe.

USIKATE TAMAA
Katika maisha watu wengi hukwama kutatua changamoto zao si kwa sababu hawana uwezo la, ila ni ile hali ya kukata tamaa mapema inapowakumba.Kwenye maisha hakuna kukata tamaa, hata kama hali ni ngumu kiasi gani usikubali kushindwa, endelea kupambana hadi tone la mwisho la jasho lako litakapoanguka ardhini, ari hii ni silaha kubwa sana ya kufanikiwa katika kupata furaha unayoitafuta.

PAZA SAUTI YA USHINDI
Watu wengi wanapokuwa kwenye hali ngumu za kimaisha hudhani kuwa watakuwa hivyo milele. Maisha yanapita, kila kwenye shida paza sauti moyoni mwako, kila mara jitangazie kuwa HILI NALO LITAPITA.

Source: Global Publishers

Monday, November 23, 2015

Rais Magufuli afuta sherehe za uhuru



sefue (2)Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ametoa taarifa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amefuta sherehe za uhuru mwaka huu na badala yake, Desemba 9 itakuwa siku ya usafi nchi nzima ili kuondokana na tatizo la kipindupindu linaoikabili nchi.
Balozi Ombeni ameongeza kuwa, wakuu wa mikoa na wilaya zote wajiandae kuandaa vifaa vya vya usafi kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Rais Magufuli ataangalia bajeti iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya sherehe hizo, kisha ataielekeza kwenye sekta au wizara  atakayoona inauhitaji ili zikasaidie kule.
“Haipendezi kusherehekea miaka 54 ya uhuru huku kipindupindu kikituua, hivyo usafi ni muhimu kwa ajili ya afya zetu,” alisema Balozi Ombeni.
Hayo yamejiri wakati Balozi Ombeni alipofanya ziara kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kukagua mashine za MRI na zile za CT-Scan na vitanda vilivyonunuliwa kutokana na agizo la Rais Magufuli kuamuru pesa zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya bajeti ya sherehe za ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano, mjini Dodoma Alhamisi iliyopita zielekezwe Muhimbili kununua vitanda vya wagonjwa.

Thursday, November 12, 2015

WAWANIA USPIKA WAANZA KUCHUKUA FOMU

Sitta 2 Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta akisaini kitabu cha wageni kabla ya kuchukua fomu za kuwania uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Ndugu Mohamed Seif Khatib.
sitta Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta akizungumza na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Ndugu Mohamed Seif Khatib mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Blandes Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Karagwe Gosbert Blandes akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Ndugu Mohamed Seif Khatib.
Nangale George Nangale akipitia fomu ya kuwania nafasi ya uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kukabidhiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Ndugu Mohamed Seif Khatib katika ofisi ndogo za CCM Lumumba.
Sonoko
Banda Sonoko akikabidhiwa fomu za kuwania nafasi ya Uspika wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Ndugu Mohamed Seif Khatib.
Rubugu Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Oganaizesheni, Ndugu Mohamed Seif Khatib akimkabidhi fomu Ndugu Simon G.Rubugu. 

Waliojitokeza mpaka sasa kuchukua fomu Makao Makuu ya CCM Ofisi Ndogo Lumumba jijini Dar ni; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, aliyekuwa mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, Leonce Mulenda, George Nangale na Profesa Costa Mahalu, Muzamil Kalokola, Banda Sonoko na Simon Rubugu.

Monday, November 9, 2015

FAHAMU MAMBO MUHIMU KUHUSU VVU/ UKIMWI

Wiki hii tunachambua Virusi vya Ukimwi (VVU) na ugonjwa wenyewe, tutaangalia hatua kwa hatua hadi mgonjwa anaonekana kuwa ana Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi).
Ili mtu ajulikane kuwa ana VVU /Ukimwi, atapitia hatua nne za lazima kama nitakavyoziainisha.
Hatua ya kwanza hujulikana kitaalam kama Primary HIV Infection ambapo mgonjwa hudumu nayo kwa wiki nne baada ya maambukizi. Watu walio katika maambuki katika hatua hii ni asilimia 20 tu ya wenye Maambukizi ya VVU ambao huona dalili za ugonjwa huu.
Mara nyingi walio katika hatua hii madaktari hushindwa kutambua kama mgonjwa amepata Maambukizi ya VVU kutokana na dalili na viashiria vyake, hufanana sana na dalili za magonjwa mengine.
Kutokana na hilo, madaktari huwa makini sana kwani aliyeambukizwa akiwa katika hatua hii, huonesha dalili kama vile kuvimba tezi yaani swollen lymph glands, kuwa na homa kali, kuumwa koo, yaani sore throat, kujihisi mchovu, kujihisi maumivu sehemu mbalimbali mwilini, kutokwa na vipele mwilini (skin rash) na pia kutapika, kuharisha au kuumwa tumbo.
Mgonjwa mwenye dalili hizo kitaalam hutajwa kuwa amepata Acute HIV Infection/Acute HIV Retroviral Infection au Seroconversion Illness. Hatua ya pili ya VVU/ Ukimwi kitaalam huitwa Clinically Asymptomatic Stage na mgonjwa hudumu nayo kwa miaka 10 na wengi wao hawaoneshi dalili yoyote isipokuwa anaweza kuwa na tezi zilizovimba, yaani swollen lymph nodes.
Lakini ukweli ni kwamba, kiwango cha VVU kwenye damu hupungua sana lakini mgonjwa anaweza kuambukiza mtu mwingine yeyote.Hata hivyo, licha ya mgonjwa kutoonesha dalili za maradhi lakini akienda kwenye vipimo vya VVU vitaonesha kwamba ana maambukizi ya ugonjwa huo katika damu yake.
Wagonjwa wa kundi hili hutakiwa kupima kwa kipimo cha wingi wa Virusi Vya Ukimwi, yaani Viral Load Test kwani VVU katika mwili wanapozaliana hujificha kwenye tezi yaani lymph nodes. Kipimo hiki pia husaidia katika kumpangia mgonjwa tiba yake.
Akitoka katika hatua hiyo, huja hatua inayoitwa kitaalam Symptomatic HIV Infection, hapa kinga za kinga ya mwili huzidi kudhoofika kutokana na kuongezeka kwa VVU kwani tezi na tishu zilizoathiriwa na VVU huharibika kutokana na maambukizi kuwa mwilini muda mrefu na virusi hao hubadilikabadilika na kuwa na uwezo zaidi wa kuathiri tishu na sehemu mbalimbali za mwili na hata kuziua seli zinazokinga mwili (Thelper Cell) kutokana na maambukizi hivyo kushindwa kuzalisha seli nyingine mpya.

MATUMIZI YA ARV’s 
Wagonjwa wengi wa Ukimwi huanza kutumia dawa za kurefusha maisha (ARV’S) baada ya kufikia hatua hii. Dawa za hizo hushambulia VVU na huanza kutumiwa wakati seli aina ya CD4 (Cluster of Differentiation), zinapopungua na kuwa kiwango cha chini sana.
Itaendelea wiki ijayo.

source: global publishers

Saturday, November 7, 2015

Wametoka chichaaaa!

Woouw!Nimependa vivazi vyao.


RAIS DKT JOHN MAGUFULI AKUTANA NA MAKATIBU WAKUU WA SERIKALI IKULU, LEo





Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bwana Rished Bade na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono na Katibu Mkuu Utumishi Mhe HAB Mkwizu na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.Kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.