HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam,
imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu
(BoT), Amatus Liyumba.
Liyumba alikuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na simu ya mkononi
wakati akiwa gerezani, akitumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya
kukutwa na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya fedha za umma katika
ujenzi wa maghorofa mawili ya jengo la BoT.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Augusta Mbando, baada ya kuridhika na upande wa utetezi.
Hakimu huyo alisema baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na upande
wa mashitaka na utetezi, ameridhika kuwa Liyumba hana hatia, hivyo
anamwachia huru.
Hakimu huyo alisema amebaini kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa
Serikali ni dhahifu, hivyo umeshindwa kuishawishi mahakama yake imuone
mshitakiwa ana hatia.
Hakimu Mbando akichambua ushahidi uliotolewa na upande wa Serikali,
alisema ni dhahifu kwani unaonyesha Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Elizabeth Kaganda, alileta simu yenye namba 0653004662 ambayo walidai
alikamatwa nayo mshitakiwa gerezani Januari 27 mwaka 2011 wakati
akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela.
Alisisitiza kuwa ushahidi wa Serikali ni dhahifu kwa sababu
umeshindwa kuionyesha mahakama simu anayodaiwa kukutwa nayo Liyumba
gerezani, namba zake zilisajiliwa na kumilikiwa na Liyumba.
“Mahakama hii inalazimika kumuona Wakili wa Serikali Elizabeth
Kaganda, kuwa ni mzembe kwa sababu alikuwa na kila sababu ya kuiomba
mahakama ipokee simu ile aina ya Nokia kama kielelezo na si kuiomba
mahakama ipokee kama utambulisho, kwa sababu shahidi wa upande wa
Serikali, Patrick, alifika mahakamani kutoa ushahidi na Wakili Kaganda
alipaswa kumwongoza Patrick aitoe simu hiyo kama kielelezo na si
utambulisho, lakini wakili huyo alishindwa kufanya hivyo,” alisema
Hakimu Mbando.
Hakimu huyo alisema kwa udhahifu huo, ulioonyeshwa na Serikali katika
kesi hiyo ni faida kwa Liyumba ambaye alikuwa akitetewa na mawakili wa
kujitegemea, Hudson Ndusyepo na Majura Magafu.
Kutokana na ushahidi huo, hakimu huyo alitangaza kumwachia huru
Liyumba baada ya kumuona hana hatia katika kesi hiyo iliyokuwa ikivuta
hisia za wengi tangu ilipofunguliwa.
Mwaka 2011 ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Liyumba akiwa gerezani
Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili jela
baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka,
alikutwa akiwa na simu hiyo gerezani kinyume cha sheria.
Ilidaiwa kuwa Julai 27, mwaka 2011 katika Gereza la Ukonga, Liyumba
alikutwa na simu kinyume cha kifungu namba 86, kifungu kidogo cha kwanza
na cha pili cha Sheria ya Magereza iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mara baada ya hukumu hiyo, Liyumba alielezea furaha yake kwamba mahakama imetenda haki.
0 comments:
Post a Comment