KIKAO cha Baraza la Madiwani cha Jiji la Arusha kimeshindwa
kufanyika baada ya madiwani kupitisha hoja ya kukaa kama kamati
wakitaka kujadili nidhamu ya Mkurugenzi wa jiji hilo, Sipora Liana,
ambaye naye aliamua kutoka pamoja na wataalamu wake akipinga
kujadiliwa.
Aidha, baada ya kutoka nje ya kikao, inadaiwa mkurugenzi huyo
alimwandikia “kimemo” Naibu Meya, Prosper Msofe (CHADEMA) aliyekuwa
akiongoza kikao hicho akimweleza hawana uwezo kisheria wa kumjadili
huku akigoma kurudi ili kuwezesha kikao hicho kuendelea.
Hayo yalitokea juzi kwenye kikao cha kawaida cha mwanzo wa mwaka cha
kupokea taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka ambacho kilikuwa
hakijaanza kujadili ajenda sita walizokuwa wamejipangia, pia Mkuu wa
wilaya, John Mongela, alihudhuria.
Hoja ya kujadili nidhamu ya mkurugenzi huyo iliibuliwa na Diwani wa
Sekei, Cripin Tarimo, (CHADEMA) ambayo iliungwa mkono na madiwani
watano na kupingwa na diwani mmoja huku madiwani wengine wakiwa
hawaungi wala kupinga hoja hiyo.
Diwani wa Viti Maalumu, Belinda Kabuje (CCM), alisimama akitaka
kupatiwa taarifa ya fedha ya Oktoba, Novemba na Desemba mwaka jana huku
akipinga kitendo cha mkurugenzi huyo kutoka nje badala ya kukaa atoe
majibu ya hoja za madiwani.
Madiwani waliwaomba waandishi wa habari kuwapisha ili wajadili suala
hilo faragha ambapo walikaa kwenye ukumbi huo kuanzia saa 5 asubuhi
mpaka saa 8 mchana.
Meya, Gaudence Lyimo ambaye aliingia kwenye ukumbi huo mkurugenzi
akiwa tayari ameshatoka alisema kuwa wamekubaliana kuandika barua ya
malalamiko kuipeleka kwenye mamlaka ya nidhamu ya mkurugenzi huyo
pamoja na kwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) na Mkuu wa Mkoa.
Alisema hiyo itawezesha Mkuu wa Mkoa (RC) kutumia mamlaka yake
kisheria kuitisha baraza la madiwani mapema kwani kwa sasa hakuna njia
nyingine.
Tanzania Daima ilipomfuata mkurugenzi huyo ofisini kwake
alijibu kupitia mmoja wa watumishi wa ofisi hiyo kuwa asubiriwe kwa
muda kabla hajabadili msimamo kupitia mtumishi mwingine akisema
hahitaji kuonana na mtu yeyote kwa muda huo. Hata hivyo majina ya
waleta majibu hayo hayakuweza kupatikana.
Sakata hili limeibuka kukiwa na mvutano mkubwa kati ya mkurugenzi
huyo kwa upande mmoja na Meya, Lyimo, Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo na
Mkuu wa Wilaya, Mongela kwa upande mwingine, hali iliyolazimu Ofisi ya
Waziri Mkuu kuingilia kati.
Chanzo: Tanzania Daima.
0 comments:
Post a Comment