“Wakazi walioko kwenye hifadhi ni lazima watii amri halali ya
Mahakama ya Rufaa na waondoke katika eneo husika. Wakati mko nje, ramani
iangaliwe upya na kubainisha wapi mipaka ipo na walio nje ya mipaka
wasibughudhiwe,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye amewasili mjini Kiteto jana asubuhi akitokea
Dodoma, alipokea taarifa fupi ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji
wilayani hapa kisha akaenda kukagua eneo husika kabla ya kuzungumza na
wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi
Kibaya.
Akitumia helikopta ya polisi, Pinda alikagua eneo husika na kuteremka
kwenye vitongoji vya Mtanzania na Laitimi, ambako aliwapa pole wananchi
waliokuwepo na kusikiliza risala katika Kitongoji cha Mtanzania.
Katika Kitongoji cha Mtanzania, watu sita waliuawa na katika
Kitongoji cha Laitimi, watu watatu waliuawa na kundi la wafugaji wapatao
40-50.
“Vitendo vilivyofanyika ni uhalifu mkubwa, nimepata taabu na
kujiuliza ni hasira za namna gani za watu kuamua kuua wakitoka kitongoji
kimoja kwenda kingine? Hii hasira inatoka wapi? Na kwa kosa lipi hasa?”
alihoji Pinda.
“Inaonekana ni kundi la watu ambao wameandaliwa wanatoka eneo moja
kwenda jingine huku wamebeba silaha. Hapana! Hali hii haivumiliki. Mkuu
wa mkoa watu hawa ni lazima watafutwe haraka sana, na kila mbinu
zitumike hadi wapatikane,” alisisitiza.
Aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kwamba kuna
masuala mengi yanazunguka suala zima la Hifadhi ya Embuley Murtangos
yakiwemo ya kuchelewesha usajili wa eneo husika, maamuzi wa kutengwa kwa
hifadhi hiyo na kutotambulika kwa mamlaka ya sheria ya ardhi ya vijiji
ya mwaka 1999.
Aliutaka uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na vijiji husika
ikae na kupanga upya matumizi ya ardhi. “Lazima mkoa na wilaya mfuatilie
mihutasari ya vijiji saba iliyopitisha uamuzi huo iko wapi ili
kujiridhisha kama maamuzi yaliyofanyika yalishirikisha wananchi wote,”
alisema huku akishangiliwa kwa nguvu na wakazi hao.
Hata hivyo, Pinda alitumia fursa hiyo kuwaeleza wakazi hao kwamba hapa nchini hakuna ardhi ambayo haina mwenyewe.
Aliutaka uongozi wa mkoa kushirikiana na makamishna wa polisi
waliofika wilayani humo kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanakuwa
salama.
“Nisingependa kusikia kuna tukio jingine wakati uchunguzi ukiendelea,” alisema.
Mapema katika taarifa yake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Elaston Mbwillo, alisema hadi kufikia Januari 13, mwaka huu watu 10
walikuwa wamepoteza maisha.
Vilevile alisema vibanda 60 vilichomwa moto, pikipiki sita na baiskeli 53 navyo pia vilichomwa moto.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment