Bahati Bukuku
Rose Muhando
STAILI, vionjo na mfumo mzima wa muziki umekuwa ukibadilika kila
siku kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ya kwenda na wakati.
Mabadiliko haya kwa upande mwingine yamekuwa sababu ya changamoto
ambazo nyingine zimeboresha mfumo mzima wa muziki kwa kunogesha, lakini
pia yameharibu.
Lakini haya yote ni kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yameikumba dunia.
Ingawa mabadiliko haya yalikwisha kutabiriwa katika vitabu
vitakatifu, lakini kwa kuwa tumekosa maarifa na macho ya rohoni, ni
vigumu kufahamu au kutambua na tumeendelea kuona kwamba ni mambo ya
kawaida.
Nimeanzia mbali kwa kuhusisha na kugusia masuala ya kiimani zaidi
na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, lakini uchambuzi wangu wa leo
utazungumzia suala la waimbaji wa nyimbo za Injili kugeuza nyimbo hizo
uwanja wa mipasho na mbwembwe za kutuonyesha kuwa wao ni mabingwa wa
kukata viuno.
Ninasema haya kwa sababu sasa hivi karibu waimbaji wengi wa nyimbo za
Injili tungo zao ni za kulalamika na kupigana vijembe, je, ndiyo
huduma mliyoitiwa?
Wengine wamepoteza ramani kabisa na kusahau talanta za uimbaji
walizopewa kwa kuanza kuimba nyimbo za dunia ambazo hazina maonyo
yoyote, hazina hata mistari ya maandiko ya kuonyana lakini bado
wanajiita waimbaji wa muziki wa Injili.
Hivi hatujiulizi ni kwanini wengine waliokuwa wakiimba nyimbo za
duniani wamehamia kwenye nyimbo za Injili na wanaimba nyimbo
zinazomtukuza Mungu kwa kumaanisha na wamefanya vizuri, wamefanyika
baraka na uponyaji kwa wengine kupitia tungo zao za muda mfupi na
kuwaacha nyuma wale wakongwe ambao wengine hivi sasa wamediriki kuwa
waimbaji kwenye kampeni mbalimbali, hasa za kisiasa huku wakipata
kashfa mbaya za kuupaka matope muziki wa Injili?
Je, mnakumbuka kwamba tulipatana dinari?
Sote tunafahamu kwamba nyimbo za Injili zipo kwa ajili ya kufundisha
na kuonya mienendo isiyompendeza Mungu kama wanadamu, lakini pia
kutuhubiria.
Lakini leo hii dhana ya muziki wa Injili imeanza kupotea kabisa
kutokana na baadhi ya tungo kujaa vionjo vya mipasho ambavyo huwemo
katika muziki wa kidunia.
Kwa mtazamo wangu, ujumbe wa neno la Mungu kufikishwa kwa staili ya
mipasho, haipendezi na haiwezi kumbadili mtu kwani huwa kama mshale.
Unaweza kujiuliza, nini maana ya kusema kama mshale? Ni ule moyo
ambao muda wote umejaa vijembe, visasi na manen0 yasiyofaa kwa ajili
ya kukera nafsi ya mwingine.
Utakuta mwimbaji wa nyimbo za Injili mwanzo hadi mwisho wa tungo
ni kulalamika na kumfumbia mtu mafumbo, jambo ambalo hata Mungu
hapendi, lakini pia hakuna hata sehemu moja anapotajwa Mungu. Je,
mtasema bado mnahubiri kwa njia ya nyimbo?
Kibaya zaidi, mnalalamika, ooh! Soko la muziki wa Injili limevamiwa, hatuuzi…mtauza nini wakati mnaimba mafyongo?
Tungo zenu hazina ujumbe ambao utanishawishi ninunue au nipende
nyimbo zenu ili hata nikiwa nasikiliza napokea upak0, uponyaji na
kupata faraja ya moyo, kwa kuwa mwimbaji alituliza akili akanena na
Roho Mtakatifu akamwongoza aimbe nyimbo za aina fulani kwa utukufu wa
Mungu.
Leo hii waimbaji wengi wa muziki wa Injili kilichobaki ni ustadi katika kucheza na kuzungusha viuno.
Yote haya yanakuja kutokana na kuimba kwa mazoea, hatumpi Roho
Mtakatifu nafasi, hatusali, hatupati maono kuhusu ni nyimbo gani za
kuimba.
Lazima tukubali kwamba hilo ni tatizo na lazima tubadilike katika hilo ili yale ambayo yamekusudiwa na Mungu yatimie.
Kwa upande mwingine, ninakubaliana na ninyi kwamba hamwezi kuimba
nyimbo za aina moja kwa sababu zinawachosha wasikilizaji lakini kila
jambo lina kiasi kama maandiko matakatifu yanenavyo.
Mbali ya yote, mnaweza kusema mbona mfalme Daudi alicheza hadi nguo zikaanguka, iweje utushambulie hivyo?
Siwashambulii, lakini pia ningependa kuwaasa kwamba ni vema
mkatambua thamani ya huduma yenu, si busara kwa mwimbaji wa nyimbo za
Injili akawa na albamu iliyobeba nyimbo ambazo hazimpi Mungu utukufu.
Kwa mtazamo wangu, ni vema waimbaji wa nyimbo za Injili mkajitambua,
mkabadilisha namna ya uimbaji ili huduma na ujumbe mliokusudia ufike
kwa jinsi ilivyokusudiwa, pia kwa kufanya hivyo mtaepuka kudharauliwa
na wapenzi wa nyimbo zenu na kurudisha imani iliyopotea.
Lakini, waimbaji wa muziki wa Injili wanapaswa kuwa mfano bora wa
kuigwa na wengine, si tu jamii bali hata wasanii wa muziki wa kidunia.
Kitendo cha baadhi ya waimbaji wa muziki wa Injili kuanza kupotoka na
kutunga nyimbo zenye mipasho, itawafanya watu washindwe kutambua nini
tofauti na muziki wa Injili na ule wa kidunia.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment