MCHAKATO wa Bunge
Maalumu la Katiba, umeanza mjini Dodoma jana ambapo wajumbe wa Bunge
hilo, walimchagua Mwenyekiti wa muda ambaye atasimamia kazi ya kuandaa
na kupitishwa kwa kanuni za Bunge hilo.
Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas
Kashililah, alimteua mjumbe wa Bunge hilo, Bi. Olivia Lwena kuwa
Mwenyekiti wa muda aliyepewa jukumu la kusimamia upigaji kura.
Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Bw. Pandu Ameir Kificho, ndiye
aliyeibuka mshindi katika uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa muda
akiwashinda wenzake wawili.
Awali, wagombea wa nafasi hiyo walikuwa
watano ambao ni Bw. David Mbatia, Profesa Costa Mahalu, Bi. Magdalena
Rubangira na Mbunge wa Jimbo la Donge, Sadifa Juma Khamis.
Bw.
Mbatia aliondolewa katika kinyang'anyiro hicho baada ya kukosa sifa za
kugombea kiti hicho ambapo Bw. Khamis, aliamua kujiondoa mwenyewe na
kuwaachia wengine.
Katika uchaguzi huo, Bw. Kificho alipata kura 393, Prof. Mahalu (84), Bi. Rubangira 84.
Wajumbe
wa Bunge hilo, walipiga kura mara mbili ambapo awali, wabunge
walihesabiwa na idadi yao kuwa 549 lakini baada ya kupigwa kura,
iliongezeka na kufikia 569.
Changamoto iliyojitokeza jana ukumbini
humo ni baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuwasha vipaza sauti bila
utaratibu baada ya kura za awali kuharibika wengine wakitaka upigaji
kura usirudiwe bali zilizoongezeka ziondolewe.
Kutokana na mabishano
ya muda mrefu, Mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro, Bw. Freeman Mbowe
alisimama na kusema kuwa, Bunge hilo linatengeneza historia, hivyo ni
vyema upigaji kura ukarudiwa.
Akizungumza baada ya kutangazwa
mshindi wa nafasi hiyo, Bw. Kificho aliwashukuru wajumbe wote kwa kumpa
kura nyingi na kuwapongeza wagombea wenzake ambao wote waliridhia
ushindi wake bila pingamizi.
Alisema kifungu cha 22 A kifungu kidogo
cha kwanza cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, pamoja na mambo mengine
jukumu alilonalo mbali ya kusimamia kazi ya kuandaa na kupitishwa
kanuni, pia atasimamia uchaguzi wa Mwenyekiti wa kudumu na makamu wake .
Aliongeza kuwa, leo kutakuwa na kikao cha kazi cha kawaida ambapo
wajumbe wa Bunge hilo watapewa rasimu ya kanuni za Bunge waweze kuisoma
na kuifahamu zaidi ambapo kikao rasmi cha Bunge hilo kitafanyika
Jumatatu Februari 24 mwaka huu, saa 3 asubuhi.
0 comments:
Post a Comment