LATEST POSTS

Wednesday, February 19, 2014

Treni ya mizigo yaanguka Morogoro na mabehewa 13

TRENI ya mizigo iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda mkoani Kigoma, imeanguka mkoani Morogoro ikiwa na mabehewa 13 ambayo yameharibika vibaya.
Chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu iliyotokea katika injini wakati treni hiyo ikiwa safarini na kusababisha irudi nyuma kwa kasi.
Akizungumzia tukio hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani humo, John Wariko alisema treni hiyo yenye kichwa namba 8906, ilianguka Februari 16 mwaka huu, saa 12 asubuhi katikati ya Stesheni ya Ngerengere na Kinonko, wilayani Morogoro.
"Mabehewa sita yalikuwa yamebeba mafuta aina ya petroli mengine yalibeba bidhaa mchanganyiko ambazo ni chumvi, ngano na saruji.
"Ni mapema mno kwa sasa kugundua hasara iliyopatikana kutokana na treni hiyo kuanguka porini hadi mizigo yote ipakuliwe tujue iliyosalimika ni ipi," alisema.
Kwa upande wake, dereva wa treni hiyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Allen Mlowe, alisema kompresa iliharibika ghafla na treni kuishiwa upepo hali iliyosababisha mabehewa kukosa breki na kuanza kurudi nyuma kwa kasi hatimaye kuanguka.
Alisema katika ajali hiyo alipata majeraha kidogo ya michubuko kutokana na msukosuko aliopata," alisema.

0 comments: