MBUNGE wa Iringa Mjini,
Mchungaji Peter Msigwa (48) (CHADEMA), amekamatwa na Jeshi la Polisi
mkoani humo akidaiwa kumjeruhi vibaya mkazi wa Itamba mjini humo, Bw.
Salum Kaita (33), ambaye ni mfanyabiashara.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ramadhan Mungi,
alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa juzi akidaiwa kumpiga nondo
kichwani Bw. Kaita ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Alisema
siku ya tukio, kulitokea vurugu katika Kata ya Nduli kwenye kampeni za
uchaguzi mdogo wa udiwani zinazoendelea baada ya mtu mmoja anayedaiwa
kuwa mfuasi wa CCM akiwa na sare za chama hicho, kuvamia mkutano wa
CHADEMA uliokuwa ukifanyika katika Kijiji cha Mgongo.
"Wakati
mkutano unaendelea, mama mmoja anayedaiwa kuwa mfuasi wa CCM, alipita
eneo hilo ndipo wafuasi wanaodaiwa kuwa wa CHADEMA, walimshambulia
wakati mkutano unaendelea.
"Pia kuna gari la CCM na wafuasi wao
ambalo lilipita eneo la mkutano huo, kukatokea kutokuelewana na
kusababisha ghasia kati ya wafuasi wa pande mbili lakini polisi
waliokuwepo eneo la tukio, waliweza kutuliza vurugu hizo," alisema.
Aliongeza
kuwa, baada ya polisi kutuliza vurugu hizo, wafuasi wa CCM walikwenda
eneo la Nduli ambapo wafuasi wa CHADEMA nao walikwenda eneo hilo
wakiongozwa na Mchungaji Msigwa baada ya kupata taarifa kuwa, CCM
wanawanunulia pombe wananchi katika moja ya kilabu.
Kamanda Mungi
alisema wafuasi wa CHADEMA na mbunge wao walipofika katika kilabu hicho
cha pombe, waliwakuta watu wawili waliokuwa wamevalia sare za CCM.
Alisema
wafuasi hao waliteremka kwenye gari na kuanza kuwapiga vijana hao
wakiongozwa na Mchungaji Msigwa ambapo tukio hilo lilishuhudiwa na mmoja
wa askari waliokuwepo katika eneo hilo.
"Askari huyu ni A/INSP
Ibrahim, ambaye kwa kushirikiana na askari wengine, walimkamata
Mchungaji Msigwa, kumuweka rumande, kijana aliyejeruhiwa yupo mahututi
na amelazwa katika Hospitali ya Mkoa," alisema Kamanda Mungi.
Aliongeza
kuwa, pamoja na wafuasi wa CHADEMA kumjeruhi kijana huyo, pia
waliiharibu pikipiki yenye namba za usajili T 209 AKH aina ya T-Better
ambayo ni mali ya Bw. Meshack Idd lakini nao walikamatwa na kufikishwa
kituoni.
Alisema katika vurugu hizo, mfuasi wa CHADEMA Bw. Alex
Mpiluka, alijeruhiwa kwenye jicho na wafuasi wa CCM, Bw. Mashaka Idd
(22) na Bw. Paulo Mapunda (56), ambao wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Msigwa afikishwa mahakamani
Ka t ika ha tua ny ing ine ,
Mchungaji Msigwa jana alifikishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa kwa tuhuma za kujeruhi.
Mchungaji
Msigwa anatuhumiwa kutenda kosa hilo juzi kwa kumjeruhi Bw. Kaita
kwenye mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea wa udiwani wa CHADEMA, kata
ya Nduli, Bw. Ayub Mwenda.
Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya, wakili wa Serikali
Elizaberth Swai alidai Februari 5 mwaka huu, katika Kata ya Nduli,
mtuhumiwa bila kukusudia alimjeruhi Kaita kinyume cha sheria sura ya 16
ya mwaka 2002 kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu.
Hata hivyo,
Mchungaji Msigwa alikana kuhusika na kosa hilo ambapo wakili Swai
aliiambia mahakama kuwa, upelelezi wa shtaka hilo haujakamilika na
kuomba mahakama ipange tarehe ya kusikilizwa tena.
Mahakama
ilikubali ombi hilo na kuipanga Machi 10 mwaka huu ambapo Hakimu Isaya
alisema dhamana ya mtuhumiwa iko wazi kwa kuwa na wadhamini wawili
ambapo Mchungaji Msigwa alitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa.
Mchungaji Msigwa alidhaminiwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa Lilian Msomba.
Jeshi
la Polisi liliimarisha ulinzi katika Kituo cha Polisi Kati ambako
Mchungaji Msigwa aliwekwa rumande pamoja na eneo la mahakama.
Askari
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa na mabomu ya machozi,
walionekana wakifanya doria eneo la mahakama na kuwataka wananchi
wasikusanyike nje ya viwanja hivyo.
Wa f u a s i wa CHADEMA
walifurika mahakamani hapo na kukaa vikundi ambapo baada ya Mchungaji
Msigwa kutoka katika chumba cha mahabusi kupelekwa kizimbani, wanachama
hao walionesha ishara ya vidole viwili.
Baada ya kupewa dhamana,
wanachama walitoka haraka nje ya jengo la mahakama ambapo wakati
Mchungaji Msingwa akitoka, wafuasi hao walimbeba juu juu na kuanza rasmi
maandamano ya kwenda katika ofisi za chama hicho Wilaya zilizopo eneo
la Mshindo.
Akizungumza na wafuasi hao, Mchungaji Msigwa alisema;
"Nawashukuru sana kwa kuniunga mkono katika kipindi hiki kigumu,
naondoka kwenda kujiandaa kwa ajili ya kwenda katika kampeni za udiwani
Nduli naomba wale wote wanaotaka kuungana nami wajitokeze," alisema.
Alisema
kesi aliyofunguliwa ni ya kisiasa na kwamba yeye wanamuonea kwa kuwa
alikuwa akizungumza jukwaani na hakumpiga mtu zaidi ya kulisikia tukio
hilo," alisema.
Chanzo: Majira
0 comments:
Post a Comment