LATEST POSTS

Wednesday, March 19, 2014

Mahabusu ajinyonga kituoni

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Mbeya likiwemo la mahabusu aliyefahamika kwa jina la Nassoro Paulo (70), mkazi wa Ruiwa, wilayani Mbarali, kujinyonga kwa kutumia shati lake akiwa ndani ya kituo cha polisi.
Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ahmed Msangi, ilisema tukio hilo limetokea Machi 17 mwaka huu, saa 10 alfajiri katika Kituo cha Polisi Kati mkoani humo.
Alisema marehemu alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za mauaji na alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo kwa matibabu.
Kamanda Msangi alisema, marehemu alikamatwa kutokana na tuhuma za mauaji anayodaiwa kuyafanya Februari 12 mwaka huu, kwa kumpiga nyundo kichwani Donald Yusuph.
Aliongeza kuwa, marehemu Paulo alifanya unyama huo kwa Donald baada ya kudaiwa kumuibia ng'ombe wake, kuuficha mwili wake sehemu isiyofahamika.
Hata hivyo, Kamanda Msangi alisema marehemu Paulo alikamatwa baada ya kupatikana ushahidi kutoka kwa watu walioshuhudia tukio la mauaji na alipohojiwa aliwaahidi wapelelezi kuwapeleka kwenye eneo alilouficha mwili huo Machi 17 mwaka huu.
"Ilipofika saa 10:50 alfajiri wakati mtuhumiwa akiwa mahabusu chumba cha pekee yake kutokana na umri wake kuwa mkubwa, alifanya jaribio la kujinyonga kwa kutumia shati lake," alisema.
Aliongeza kuwa, askari wa zamu walifika na kumkuta chini akipumua kwa shida hali iliyowafanya wamkimbize Hospitali ya Rufaa kwa matibabu ya haraka lakini hakuweza kuchukua muda mrefu hatimaye alifariki dunia.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Mnazi, Mchimbi Aladi (34), Tarafa ya Rujewa, wilayani Mbarali, amefariki dunia baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na watu wasiofahamika.
Kamanda Msangi alisema watu hao baada ya kumpiga marehemu na kuhakikisha kuwa amefariki, waliutupa mwili wake katika Mto Ruaha ambapo tukio hilo limetokea Machi 16 mwaka huu, katika Kitongoji cha Igunula, Kijiji cha Mnazi.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni tuhuma za uchawi ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Innocent Nkwanda (24), mkazi wa Mbozi, amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Ametoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria.

0 comments: