Chama Cha Mapinduzi kimezindua kampeni katika Jimbo la Chalinze kwa kishindo, huku viongozi wa kitaifa wakimwombea kura, Ridhiwani Kikwete ili awaletee maendeleo.
Akizindua kampeni hizo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema CCM ni chama chenye kuleta majawabu kwa Watanzania, hivyo wananchi wasikubali kurubuniwa na wapinzani.
“Tunatambua kwamba hapa hatushindani na upinzani bali tunashindana na matatizo ya wananchi, na kwa Chalinze atakayesimamia hilo ni Ridhiwani Kikwete,” alisema.
Alisema Ridhiwani ni mgombea kijana, atakayeweza kukaa na vijana kutatua kero zao kwa karibu kuliko mtu mwingine, hivyo wamchague kwa kura nyingi za kishindo.
Aliwataka vijana wawe karibu na Ridhiwani, kwa kuwa CCM inajipanga kuhakikisha kazi zote za ukandarasi wapatiwe vijana hivyo utaratibu utakapopangwa, mbunge ndiye atakuwa kiunganishi.
“Chagueni mbunge ambaye atatatua matatizo ya wananchi, atakayekwenda kuungana na asilimia 74 ya wabunge wa CCM kufanya kazi za wananchi,” alisema.
Kinana alisema CCM inatambua matatizo ya Jimbo la Chalinze ikiwemo tatizo la maji, ambalo Ridhiwani atakuwa na nafasi kubwa ya kuendeleza yale yaliyoachwa na aliyekuwa mbunge, Said Bwanamdogo aliyefariki hivi karibuni.
Katika mkutano huo, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete aliwataka Wanachalinze kutomuumiza tumbo kwa kumnyima ridhaa mwanaye Ridhiwani ambaye anaamini atatatua kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.
Mama Salma alitoa ombi hilo katika viwanja vya Polisi Chalinze, kuwa yeye kama mama mzazi ana kila sababu ya kumwombea kijana huyo kura zote za ndiyo kutokana na kuwa na uwezo wa ushawishi wa masuala mbalimbali na pia ni mpenda watu popote alikokuwa akipita.
Alisema amefika katika viwanja hivyo kwa sababu kuu tatu, moja ni mama mzazi wa mgombea, pili ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Lindi na tatu ni kwa vile yeye ni mke wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
“Ndugu zangu Wanachalinze, leo tumbo linaniuma sababu ya mwanangu, lakini namjua mtoto wangu ni mpenda watu, popote alikopita alieneza upendo na pia ana uwezo mkubwa wa kuongoza na kujenga ushawishi wa masuala mbalimbali ya maendeleo,” alisema na kuongeza:
“Nawaomba sana msiniangushe mzazi mwenzenu, kihemba na mwanaye na pia uchungu wa mwana ajue mzazi namwombea kura zote Ridhiwani,” alisema Mama Salma.
Akizungumza kabla ya Kinana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema CCM kitaendelea kuendesha kampeni za kistaarabu lakini waliozoea fujo wakithubutu hawatavumiliwa.
“Tunajua kwamba ni wasindikizaji lakini katika kusindikiza wakitufanyia fujo watakiona cha mtema kuni, lakini tumejipanga kufanya kampeni za kistaarabu,” alisema.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alimnadi Ridhiwani akisema ni kijana aliyelelewa kwenye maadili, hivyo hana shaka.
Alitumia lugha ya Kimasai kuwashawishi wafugaji wa asili ya Kimasai wamchague Ridhiwani kwa kuwa anayetafutwa ni mbunge na sio kiongozi wa kimila.
“Hapa tunafanya kampeni ya kumchagua mbunge sio kiongozi wa kimila, hivyo msihadaike na mgombea wa Chadema, kwa kuwa hatoshi ubunge labda kiongozi wa kimila,” alisema.
0 comments:
Post a Comment