Asubuhi imewadia, milio ya mageti yanayofunguliwa inasikika mtaani.
Ni mtaa uliopo mjini katika kitongoji kimoja wanachoishi watu wenye uwezo mzuri wa fedha.
Milio ya mageti haya asubuhi hii ni ishara kuwa wenyewe wanatoka kwenda kuwajibika. Hata hivyo, karibu kila gari linalotoka katika mageti ya mtaa huu, ndani kuna mtoto au watoto wawili watatu hivi wa shule.
Katika nyumba moja, watoto wawili wanakimbia kuelekea getini. Nje kuna gari dogo la kifahari likiwasubiri. Wakiwa na sare nadhifu na miili iliyonenepa, watoto hao wanahimizwa na dereva kuharakisha hatua zao.
Watoto hawa na wengine mtaani hapo, wanakwenda shule. Wapo watakaopelekwa moja kwa moja shuleni, wapo watakaoshushwa njiani kusubiri ‘magari ya njano’, ambayo ni maarufu kwa kusafirisha wanafunzi mijini.
Kwengineko muda huohuo katika kijiji kimoja maskini jirani na mgodi maarufu wa dhahabu, watoto kadhaa wa shule za msingi wakiwa na sare chakavu na chafu, huku miguu yao ikisitiriwa na viatu maarufu kwa jina la ‘yeboyebo’, wameanza nao safari ya kwenda shule.
Ni safari ya kilometa zisizopungua nne inayowalazimu kupita vichakani, porini na pia kupanda na kushuka vilima kadhaa njiani.
Ni safari ndefu na ya kuchosha kwao ambayo mara nyingi inawafanya wafike shuleni wakiwa wamechelewa. Hawana jinsi watoto hawa, hayo ndiyo maisha ya kila siku kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa .
Aghalabu katika safari yao kwenda shule, watoto hawa hutumia muda mwingi wakishangaa magari na vifaa vya kuchimbia madini katika mgodi ulio jirani na kijiji chao.
Wanawashangaa ‘wajanja’ wakichimba kile wasichokijua kuwa kingeweza kuwasaidia wazazi wao kuwanunulia sare na viatu bora, au hata kujengewa shule jirani na makazi yao.
Tofauti ya watoto hawa
Watoto wale wa mjini na hawa wenzao wa kijijini, wote asubuhi hii wanaelekea shuleni, mahala wanapokwenda kupata haki ya msingi ya kujielimisha kama wanadamu.
Hata hivyo, shule wanazosoma watoto hawa zinatofautiana kwa kiwango kikubwa na zile zilizopo vijijini. Shule za walio nacho mijini zina mazingira rafiki, ya kisasa na bora kwa ufundishaji na ujifunzaji.
Shule hizi zinazoitwa za watoto wa vigogo, ndizo wanazosoma pia watoto wa watendaji wakuu serikalini, wakiwamo wale waliokabidhiwa jukumu la kuboresha elimu katika shule za wasionacho kule kijijini.
Mazingira ya shule hizi zinazojulikana kwa majina kama vile ‘academy’ , ‘international schools’ yana sifa zifuatazo: 1. madarasa bora na yenye uwiano mzuri wa walimu na wanafunzi, yaani mwalimu mmoja kwa wanafunzi wasiozidi 35. 2.Zina walimu wenye sifa na hamasa ya kufundisha, kwa sababu wamiliki wake wanajali hadhi na maslahi ya walimu.
3. Zina madarasa yaliyosheheni vifaa vya kisasa kama vile kompyuta, projekta na vinginevyo. 4. Maktaba zimejaa vitabu na kila aina ya majarida muhimu kwa taaluma. 5. ‘Kiswahili cha dunia’ yaani Kiingereza ndiyo lugha kufundishia na ya mawasiliano katika shule hizi.
0 comments:
Post a Comment