MTU mmoja anayedaiwa kuwa jambazi sugu maarufu kama Ramadhani Jumanne
‘Rama Ndonga’ (37) ameuawa katika majibizano ya risasi kati yake na
polisi yaliyotokea usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Moivo,
Arumeru mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
(SACP), Liberatus Sabas alisema, kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa
kwa muda mrefu kutokana na kuhusika katika matukio mbalimbali yakiwemo
ya mauaji ya Sakina.
Kamanda alisema kuwa polisi walitumia mbinu za kipelelezi na kufika
nyumbani kwa mtuhumiwa usiku wa manane na kumwamuru marehemu (mtuhumiwa)
kujisalimisha lakini alikaidi na kuanza kuwarushia risasi hatua
iliyopelekea kujibu mapigo na kusababisha kifo chake.
Alisema kuwa marehemu alihusika katika matukio mbalimbali likiwemo
lililotokea Agosti 21, mwaka huu ambapo akiwa eneo la Olasiti alimjeruhi
kwa risasi mtoto mdogo Christen Nickson (3) kwa kumpiga risasi mdomoni
iliyotokea kichwani na kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika
hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Alisema kuwa polisi walifanya upekuzi nyumbani kwa marehemu na
kufanikiwa kukuta bastola aina ya Glock 19 yenye namba RLU976
iliyotengenezwa nchi Australia ikiwa magazine yenye risasi 14.
Kamanda alisema pia marehemu alipatikana na magazine moja yenye
risasi 15 na magazine mbili zenye uwezo wa kubeba risasi 30 kila moja,
redio ya upepo yenye namba ITSS/UNICTR inayodaiwa kuporwa kwenye
mahakama ya kimbari ya Rwanda.
“Alikutwa na pikipiki aina ya Toyo Power King yenye namba T.507 BSU,
kofia ngumu ya kuendeshea pikipiki, pingu pamoja na vifaa vya kusafishia
bastola na koti jeusi,” alisema
0 comments:
Post a Comment