KITUO cha Redio Times FM,kimetakiwa kulipa faini ya shilingi milioni
moja baada ya kukiuka sheria ya utangazaji kwa kurusha vipindi vya ngono
muda ambao haurusiwi.
Hukumu hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na kamati ya maudhui
ya utangazaji, katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano na Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Margaret Munyagi.
Munyagi alisema vipindi vilivyokiuka maadili hayo ni kile cha ‘Hatua
Tatu’ kinachorushwa kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 5 na kipindi cha
mitikisiko ya Pwani kinachorushwa saa 6 mchana hadi 10 jioni.
Akifafanua zaidi makosa hayo, alisema katika kipindi cha ‘hatua
tatu’, watangazaji katika kipengele cha hatua za afya walikuwa
wakiongoza mjadala wa mada ya kufanya ngono mara mbili kwa wiki
kunamwezesha binadamu kuishi muda mrefu.
Huku yule anayefanya ngono mara moja kwa mwezi kuwa katika hatari ya kuishi muda mfupi.
Katika mjadala huo, inaelezwa kuwa watangazaji walionekana wazi
kushabikia ikiwemo kuulizana wenyewe kuwa huwa wanafanya ngono mara
ngapi, kitu ambacho ni kinyume na maadili ya utangazaji kwa kuzungumza
mambo hayo muda wa mchana.
Mwenyekiti huyo alisema ni hatari kwa kuwa wakati huo wasikilizaji
wengi ni watoto jambo ambalo linaweza kuchangia kuzalisha kizazi
kisichokuwa na maadili.
Wakati kwa upande wa kipindi cha Mitikisiko ya Pwani, Mtangazaji
alikuwa akizungumzia mada ya msichana aliyefumaniwa baada ya kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na mjomba wake.
Kutokana na makosa hayo alisema walisikiliza ushahidi kupitia CD za
vipindi hivyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wasikilizaji na
kujidhirisha kuwa walikuwa wamekosea.
Pia alisema waliwaita upande wa walalamikiwa akiwemo Mkurugenzi wa
Times FM, Richard Nyaulawa na Mkuu wa Vipindi wa kituo hicho, Hemes
Joachim, ampapo wote walikiri makosa hayo.
Kwa mujibu wa Munyagi faini hiyo watatakiwa wailipe ndani ya siku 30
kuanzia jana na imeenda sambamba na onyo kali dhidi ya kituo hicho.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment