LATEST POSTS

Saturday, August 24, 2013

TUTAANIKA MAJINA YA WAKURUGENZI NA WAHASIBU 70 WANAOTAFUNA FEDHA ZA UMMA YASEMA KAMATI YA HESABU ZA SERIKALI (LAAC)

`

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), imesema itaweka hadharani majina ya wakurugenzi na wahasibu 70, ambao ni ‘mchwa’ wa fedha za umma kwenye halmashauri.
Kadhalika, Kamati hiyo imebaini kuwapo kwa mtandao wa ‘mchwa’ hao kati ya wakurugenzi, wahasibu na baadhi ya vigogo wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Hazina katika kutafuna fedha hizo.
Kamati hiyo pia imepanga kumwita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na Naibu Waziri wake, ili kuweka wazi vikwazo wanavyokumbana navyo katika kuwashughulikia wakurugenzi na wahasibu hao.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajabu Mbarouk Mohamed, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandsihi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo kukutana na wakurugenzi wa baadhi ya halmashauri.

Aidha, Kamati hiyo imesema kuna harufu ya rushwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kuwa imekuwa ikiendesha uchunguzi wa kesi za ubadhirifu kwa miaka mingi pasipo kuwafikisha mahakamani wahusika na wakati mwingine kwa miaka mitano.

Alisema tatizo kubwa ni uhamisho unaofanyika mara baada ya kubainika ufisadi kwenye halmashauri badala ya kuwachukulia hatua na wakati kamati ikijiandaa kwenda kuitembelea, watumishi husika huamishwa kwa haraka.

“Inashangaza wakati kamati tunajiandaa kwenda kwenye Halmashauri fulani, tayari wanataarifa na uhamisho unafanyika kwa haraka, tunapofika wahusika hawapo na tunakosa majibu ya hoja tulizonazo,” alisema.

Alisema awali wakati Kamati hiyo ikiwa chini ya Mwenyekiti Augustino Mrema, aliagiza serikali kuacha kuwahamisha kwenye maeneo mengine wale wote wanaodaiwa kuhusika na ubadhiliufu wa fedha za umma, lakini kwa wakati huu kasi ya kuhamisha imezidi.
 
Alisema kamati hiyo imefika mahali pa kushindwa kufanyakazi zake na sasa imeamua kumweleza Waziri Mkuu na Waziri husika.  Mbarouk bila kutaja takwimu, alisema Halmashauri za Mbulu na Arusha kuna ubadhirifu wa hali ya juu uliofanyika kwa miaka 10 na mbaya zaidi wamekataa kutoa ushirikiano kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
"Wameshindwa kumpa vielelezo husika CAG, tumewaita mbele ya Kamati wameshindwa kujieleleza, wameficha vielelezo, hoja nyingi ni za miaka ya nyuma ambazo wahusika ni Wakurugenzi na Waweka Hazina (wahasibu) ambao wameshahamishwa siku nyingi na kuendelea na kazi kwenye halmashauri nyingine," alisema.  Alisema kwenye Halmashauri hizo wameshindwa kupeleka vijijini fedha za miradi mbalimbali na badala yake zimetumika pasipo taarifa za kueleweka.
 
Mathalani, alitolea mfano wa Halmashauri ya Mwanza, kamati ilikwenda na kukuta mkurugenzi na mwekahazina wamehamishwa mmoja jijini Dar es Salaam na kamati kukosa majibu ya maswali yaliyoulizwa kwa kuwa waliokuwapo hawakujua lolote.
"Tulishangazwa na baada ya utafiti wetu tulibaini kuwa kuna mtandao mrefu kati ya Hazina na Tamisemi kwenye kuwahamisha vituo vya kazi watumishi husika," alisema.
 
Mbarouk alisema yapo yanayofanyika yanayoingiza serikali gharama kama uhamisho wa mara kwa mara wa watumishi hao na katika Halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani, serikali inagharimia wakurugenzi wawili na waweka hazina wawili ambao wako kazini na mapumzikoni.  
Aidha, alisema wameagiza halmashauri nchini kutoza mapato kwa kutumia stakabadhi za elektroniki ili kuongeza mapato ya serikali na hilo linatekelezwa katika Manispaa ya Temeke na mapato yameongezeka.
Alibainisha kuwa Kamati imemwagiza CAG kutokagua stakabadhi zilizopo katika muundo wa kuandikwa kwa mkono na badala yake za mfumo wa elektroniki. Alisema zimebaki halmashauri 11 kukutana na kamati hiyo na leo watakutana na ya Korogwe na Korogwe Vijijini ambayo imekuwa ikifanya vibaya kwa miaka mitano. 
Alisema Kamati yake itakutana na waandishi wa habari Agosti 23, mwaka huyu, kwa ajili ya kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwamo kutaja majina ya wakurugenzi na waweka hazina wanaoongoza kwa ubadhilifu nchini.
 Katika hatua nyingine; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), imemwagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hasa katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gaudence Kayombo alisema jana alipokutana na viongozi wa wizara hiyo kuwa kuna matumizi makubwa ya fedha katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
“Kamati itamwandikia CAG, afanye ukaguzi maalumu ili kubaini utata unaoonekana katika matumizi ya fedha ya wizara hiyo hasa kwenye eneo la mikutano,” alisema Kayombo.
Kayombo alisema kutokana na utata huo, kamati imeona haiwezi kuijadili ripoti hiyo ya fedha ya mwaka 2012/13 hadi CAG atakapofanya ukaguzi maalumu.
Aidha, Kayombo aliwataka viongozi hao wataje gharama za Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliojengwa kwa mkopo na msaada wa Serikali ya China, lakini Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Haule alisema ataitaja baadaye baada kujiridhisha.
“Tunataka kufahamu gharama za ujenzi wa jengo hilo, vifaa vilivyosamehewa kodi ili kamati iweze kujua, kwa sababu hadi sasa haieleweki umegharimu kiasi gani,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, alisema asilimia 46 ya gharama za ujenzi wa jengo hilo ni msaada wa Serikali ya China huku asilimia 54 ikiwa ni mkopo.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz na Nipashe

0 comments: