Dar es Salaam. Mtanzania anayeishi Afrika Kusini, Stephen Ongolo amekamatwa na polisi wa nchi hiyo akidaiwa kutishia kutoa siri za mke wa pili wa Rais Jacob Zuma, Nompumulelo Ntuli Zuma au MaNtuli.
Kwa mujibu wa magazeti ya Sunday Times na
Independent ya Afrika Kusini, Ongolo alikamatwa Ijumaa, Januari 24 na
alitakiwa kufikishwa katika Mahakama ya Durban juzi kabla ya kusogezwa
hadi wiki ijayo.
Kabla ya kukamatwa, Ongolo aliwasiliana na
magazeti mbalimbali nchini humo akidai kuwa amekuwa akilipwa, Randi
200,000 (Sh29 milioni) kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ili afiche siri za
mke huyo wa Rais.
Katika madai yake, Ongolo alisema mke wa Zuma,
(MaNtuli), amekuwa akimtumia ili kupata kibali cha uchimbaji wa madini,
nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa mujibu wa magazeti hayo, kabla ya kukamatwa,
Ongolo alidai kuwa anafahamu taarifa za MaNtuli kwa kina na anajipanga
kuzitoa kwenye vyombo vya habari.
Alidai kuwa kuna siri kubwa ya urafiki wa MaNtuli
na aliyekuwa mlinzi wake, Phinda Thomo ambaye alijiua kwa kujipiga
risasi bafuni kwake, Soweto mwaka 2009.
Magazeti hayo yalimkariri Ongolo kupitia barua
pepe, akisema kifo cha Thomo hakikuwa cha kujiua, bali mauaji ya
kupangwa yaliyosababishwa na uhusiano wa siri kati yake na MaNtuli.
Iliwahi kuripotiwa kwamba Thomo alijiua baada ya kugundua kuwa vyombo vya habari vinachunguza uhusiano kati yake na MaNtuli.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia
Msuya alisema wamepata taarifa hizo kwa mshtuko na ofisi yake
inafuatilia kujua kweli kuhusu uraia wa Ongolo.
“Ubalozi haufahamu kuhusu uraia wake. Baada ya
kupata taarifa hizo tunachokifanya sasa ni kufanya uchunguzi kama kweli
ni raia wa Tanzania kisha tutawaeleza,” alisema.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna,
Abbas Irovya alisema watawasiliana na ubalozi kuthibitisha kama Ongolo
ni Mtanzania.
Siri kuhusu Thomo
Mtanzania huyo alizungumza na Gazeti la Sunday Times na kudai
kuwa kuna vitu ambavyo Thomo alivifahamu ambavyo MaNtuli hakutaka
viwekwe wazi.
“Kama Thomo angekuwa hai, angeleta changamoto
kubwa kuhusu suala la mtoto,” alisema Ongolo. MaNtuli alipata mtoto
katika kipindi ambacho Thomo alijiua.
Ongolo alidai kuwa yeye ni rafiki mkubwa wa
MaNtuli na mara kadhaa amewahi kupata chakula cha mchana na Rais Zuma
katika jumba lake la Nkandla na amekuwa akitumia gari la Serikali la
MaNtuli.
Mei 17, mwaka jana kwenye ukurasa wake wa
Facebook, Ongolo aliandika: “Kwa marafiki zangu, ninatarajia kwenda
Afrika Mashariki, naanzia Zimbabwe, Zambia na safari yangu itaishia
Tanzania, nyumbani”.
Kadhalika, Agosti 31 mwaka jana aliandika maneno
haya kwenye ukurasa huo: “Mungu ambariki dada na rafiki yangu MaNtuli
Zuma na mume wake Jacob Zuma”.
Ongolo aliongeza kuwa ameamua kuweka wazi ukweli kwa sababu amechoka kupokea ujumbe mfupi wa vitisho kutoka kwa MaNtuli.
Alitoa hadharani ujumbe mfupi ambao alidai umetoka
kwa mke huyo wa Rais ambao ulisomeka: “Stephen, unachonifanyia si
kizuri. Nilikuchukulia kama kaka, nilikuamini na kukupa siri zangu, sasa
hivi unanigeuka. Nimefanya kosa gani?
Badili fikra zako usizungumze na vyombo vya dola
kwa sababu haitaniharibia mimi bali hata mume wangu. Maadui zangu wapo
kazini lakini si wewe Stephen. Nina pesa za kubadili maisha yako.
Fikiria.”
Ongolo alipoulizwa kwa nini ameamua kusema hayo hivi sasa alisema anahofia maisha yake na anataka ukweli uwekwe wazi.
0 comments:
Post a Comment