LATEST POSTS

Saturday, February 1, 2014

Uamsho wapewa dhamana ngumu

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/02/uamsho.jpg

MAHAKAMA Kuu mjini Zanzibar imetoa dhamana ya masharti magumu kwa watuhumiwa wa uchochezi ambao ni viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu.
Watuhumiwa hao ni Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) mkazi wa Mbuyuni, Mselem Ali Mselem (52) mkazi wa Kwamtipura, Mussa Juma Mussa (47) mkazi wa Makadara na Azan Khalid (48) mkazi wa Mfenesini.
Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66) mkazi wa Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) mkazi wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakar Suleiman (39) mkazi wa Tomondo, Ghalib Ahmada Juma (39) mkazi wa Mwanakwerekwe, Abdallah Said (48) mkazi wa Misufini na Majaliwa Fikirini Majaliwa.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji wa mahakama hiyo, Fatma Hamid Mahmoud, amewataka kuwasilisha fedha taslimu sh milioni 25 kila mmoja, wadhamini watatu lazima wawe wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kati yao mmoja awasilishe mali isiyohamishika yenye thamani ya sh milioni 25.
Mashati mengine ni kuwasilisha vitambulisho na hati za kusafiria mahakamani hapo, kutotoka nje ya Zanzibar, kutofanya mihadhara ndani na nje ya misikiti, kutofanya vitendo vyovyote vyenye kuashiria fujo, kinyume cha hapo watarudi rumande hadi kesi itakapokwisha.
Mwendesha mashtaka wa serikali, aliwasilisha pingamizi mbele ya jaji huyo kuzuia amri ya kuwataka kuwasilisha sababu za kuzuia dhamana za watuhumiwa hao.
Mashtaka waliyosomewa washtakiwa hao ni kuharibu mali, uchochezi, ushawishi na kuhamasisha fujo na kosa la tatu ni kula njama ya kufanya kosa.
Kosa la nne likimkabili mshitakiwa Azan Khalid
anayedaiwa kutoa maneno ya matusi kwa kamishna wa polisi vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Vitendo hivyo vinadaiwa kufanyika kati ya Oktoba 17, 18 na 19 kwenye maeneo tofauti katika Manispaa ya Mji wa Zanziba ambapo washtakiwa wote walikana makosa yao.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februai 27, mwaka huu na watuhumiwa walirudi rumande hadi watakapokamilisha masharti ya dhamana zao.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: